Safari ya Macron barani Afrika; juhudi za kueneza ushawishi
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa yuko barani Afrika katika safari yake ya kwanza ya kikazi baada ya kuanza muhula wake wa pili kama rais wa nchi hiyo.
Lengo la safari ya Macron katika nchi kadhaa za Afrika limetajwa kuwa ni kujadiliana na viongozi wa nchi hizo kuhusu masuala ya usalama, mzozo wa chakula na jinsi ya kupanua uhusiano wa Ufaransa na nchi za Afrika. Katika safari hiyo, rais wa Ufaransa ambaye kwanza aliwasili Yaounde, mji mkuu wa Cameroon, amepangiwa kuzitembelea pia nchi za Benin na Guinea-Bissau. Safari ya Macron inakuja wakati ambapo raia wengi wa nchi hizo hawajaridhishwa na utendaji wa Ufaransa katika bara hilo, huku uhalifu na jinai zake zikisalia hai katika kumbukumbu zao za kihistoria.
Badimo Ko, mwanachama wa Vuguvugu la Afrika la Uhuru na Demokrasia Mpya (MANIDEM), anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Tuna mzozo wa kihistoria na Ufaransa. Sio kuwasili kwa Macron ndiko kunaleta matatizo. Tutatumia fursa hii kuwafahamisha wananchi wa Cameroon kuhusu matatizo ya Ufaransa, ambapo tunataka kuweka jinai zote za Ufaransa mezani na kuzitatua kabisa.

Hata kama nchi za Kiafrika ziliifukuza Ufaransa katika nchi hizo kupitia mapinduzi dhidi ya ukoloni katika karne zilizopita, lakini katika miongo ya karibuni Ufaransa imekuwa ikiimarisha uwepo wake barani humo kwa visingizio tofauti. Kisingizio muhimu zaidi ambacho kimekuwa kikitumiwa na nchi hiyo ya Magharibi katika uwanja huo ni kuwa eti inataka kuzisaidia nchi za Kiafrika na hasa za Magharibi na katikati mwa Afrika kuweka usalama na kupambana na ugaidi. Kwa msingi huo, katika miaka mitano iliyopita, Ufaransa imeimarisha uwepo wake barani Afrika na hasa katika eneo la Sahel, kituo chake muhimu cha kijeshi kikiwa Mali. Jeshi la Ufaransa limeifanya Mali kuwa kituo chake kikuu na ina udhibiti kamili juu ya nchi za eneo hilo. Bila shaka, katika miezi ya karibuni na kufuatia mabadiliko ya kisiasa barani Afrika na hasa Mali, Ufaransa imelazimika kuondoa wanajeshi wake katika nchi hiyo.
Hata hivyo, viongozi wa Ufaransa ambao hawataki kuipoteza Afrika, wametangaza rasmi kwamba jeshi la Ufaransa litatumwa katika nchi nyingine za bara hilo. Sasa, moja ya malengo muhimu ya Macron ni kutafuta nchi ambayo itakubali kuwapokea askari hao. Katika safari hiyo, Macron amesisitiza tena nia yake ya kurefusha "Mchakato wa Kijeshi na Kiusalama" wa Ufaransa, haswa katika eneo la Sahel, na kudai kwamba Ufaransa 'haitapuuza usalama wa bara la Afrika.'
Macron pia ametangaza kuwa kuimarishwa majeshi ya kikanda na kustawishwa ushirikiano katika uga wa usalama, ulinzi na diplomasia ni miongoni mwa hatua za baadaye za Ufaransa katika bara la Afrika.
Madai ya Macron yanatolewa huku nchi za Kiafrika zikiwa haziridhishwi na utendaji kazi wa Ufaransa, na askari wake badala ya kuweka usalama ndio kwanza wanahusika na mauaji ya raia wa nchi tofauti barani humo. Nchini Mali, raia wengi wa nchi hiyo wameuawa na vikosi vya Ufaransa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Katika upande mwingine, Afrika ni muhimu sana kwa Ufaransa, hivyo viongozi wa Paris wana hofu na wasiwasi mkubwa kuhusu kuenea ushawishi wa washindani wao katika nchi za Afrika; hasa katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi za Kiafrika haziungi mkono msimamo wa nchi za Magharibi dhidi ya Russia kuhusiana na vita vya Ukraine. Hivyo, Ufaransa inajaribu kila njia ili kuzishawishi nchi hizo zikubaliane na siasa zake barani humo na kuhusu masuala muhimu ya kimataifa.

Kwa kuongezeka mgogoro wa chakula, nchi za Kiafrika sio tu kwamba hazikubaliani na sera za Magharibi dhidi ya Russia, bali zinaamini kuwa vikwazo na uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine ndio umesababisha upungufu wa chakula duniani na hivyo kuharibu zaidi hali ya mambo barani Afrika.
Katika muktadha huo, Macron amejaribu kuhalalisha hatua za nchi za Magharibi dhidi ya Russia na kudai kuwa chakula kama ilivyo nishati, kinatumiwa na nchi hiyo kama silaha. Hata hivyo na kama ilivyokuwa huko nyuma, haionekani kuwa nchi za Kiafrika zinakubaliana na sera za Paris kuhusu matukio mengi ya kimataifa na kikanda.