Aug 03, 2022 12:04 UTC
  • Israel yaruhusiwa kujenga ubalozi Morocco licha ya pingamizi la wananchi

Utawala wa Kizayuni wa Israel umedai kuwa umesaini mkataba wa kuuruhusu ujenge ubalozi nchini Morocco, licha ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi.

David Govrin, balozi wa Israel nchini Morocco amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "Nina furaha kusambaza hii picha inayoonesha lahdha ya kihistoria ya kutiwa saini makubaliano ya kuanzisha ubalozi wa kudumu nchini Morocco."

Amedai kuwa, kujengwa jengo la ubalozi wa kudumu wa Israel nchini Morocco kutafungua ukurasa mpya katika uhusiano wa Tel Aviv na Rabat.

Haya yanajiri huku maelfu ya wananchi wa Morocco wawakiendeleza kampeni katika mitandao ya kijamii ya kutaka mwakilishi huyo wa Israel nchini Morocco atimuliwe mara moja.

Katika miezi ya hivi karibuni, wananchi wa Morocco wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo na kutangaza tena kupinga nchi yao kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Balozi wa Israel asiyetakiwa na wananchi wa Morocco

Disemba mwaka 2020 Morocco ilijiunga na UAE, Bahrain na Sudan katika kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani.

Mapatano hayo yanaendelea kulaaniwa ndani ya nchi hizo za Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla kwani ni usaliti kwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

Tags