WHO yachunguza dawa za India baada ya watoto 66 kuaga dunia Gambia
Shirika la Afya Dunia (WHO) limetoa indhari kuwa, yumkini dawa aina nne za kukabiliana na kikohozi na mafua zilizotengenezwa na kampuni ya India ya Maiden Pharmaceuticals zimesababisha vifo vya watoto 66 nchini Gambia.
WHO ilitoa indhari hiyo jana Jumatano na kueleza katika taarifa kuwa, dawa hizo za watoto zinazoshukiwa kuwa na madhara kwa watoto ni Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, dawa hizo zinahusishwa na kusababisha madhara makubwa kwa figo na kupelekea watoto 66 kufariki dunia nchini Gambia.
Mkuu huyo wa Shirika la Afya Dunia ameeleza kuwa, kufariki dunia watoto hao wadogo kumewavunja moyo watu wa familia hizo, na kwamba WHO inaendelea kufanya uchunguzi ikishirikiana na mamlaka husika nchini India.

Amesema kufikia sasa, kampuni hiyo haijaipa WHO dhamana juu ya usalama na viwango stahiki vya dawa hizo zilizozalishwa na kampuni ya Maiden Pharmaceuticals ya India.
Mwezi uliopita, Wizara ya Afya ya Gambia iliziagiza hospitali za nchi hiyo ziache kutumia dawa hizo za kunywa za kukabiliana na mafua na kikohozi, baada ya watoto 28 kuaga dunia kutokana na matatizo ya figo.