Burundi yafungua mipaka yake na Rwanda baada ya miaka 5
(last modified Mon, 24 Oct 2022 04:02:28 GMT )
Oct 24, 2022 04:02 UTC
  • Burundi yafungua mipaka yake na Rwanda baada ya miaka 5

Serikali ya Burundi imetangaza kufungua mipaka ya ardhini ya nchi hiyo na jirani yake Rwanda, baada ya kufungwa kwa kipindi cha miaka mitano.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi imesema katika ujumbe wa Twitter kuwa: Mipaka yote ya Burundi na majirani zake imefunguliwa. Burundi ni nchi inayofikika.

Kwa mujibu wa mamlaka za Burundi, kibali kilichokuwa kikitolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo cha kusafiri kwenda Rwanda kutoka Burundi hakitahitajika tena.

Mataifa hayo jirani hayajakuwa na uhusiano mzuri kwa miaka kadhaa sasa, Burundi ikifunga mipaka yake; na Rwanda ikipiga marafuku uuzaji wa matunda na mboga za Burundi jijini Kigali tangu mwaka 2016.

Hata hivyo tangu kuingia madarakani kwa Rais Evariste Ndayishimiye mwaka 2020, uhusiano kati ya Kigali na Bujumbura umeonekana kuimarika kwa kiasi kikubwa.

Bendera za Burundi na Rwanda

Mei mwaka huu, Rais wa Burundi alisema kuwa, uhusiano wa nchi yake na Rwanda utakuwa mzuri zaidi iwapo watu waliopanga na kufadhili jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya 2015 wanaodhaniwa kuwa wako mafichoni jijini Kigali watarejeshwa mjini Gitega kufunguliwa mashtaka.

Waziri Mkuu wa Rwanda Edouard Ngirente, alifanya zaira jijini Bujumbura wakati wa sherehe za Siku ya Uhuru wa Burundi Julai 2021. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu wa Rwanda kuzuru Burundi tangu mzozo kwa kisiasa kuanza kati yao mwaka 2015.