Feb 04, 2023 07:26 UTC
  • Watu 40 wauawa katika mapigano jimboni Katsina, Nigeria

Watu zaidi ya 40 wameuawa katika mapigano baina ya kundi la wabeba silaha na wanakijiji waliojitolea kulinda usalama katika jimbo la Katsina, kaskazini mwa Nigeria.

Msemaji wa Polisi katika jimbo la Katsina, Gambo Isah alisema jana Ijumaa kwamba, genge la wabeba silaha wanaotambulika nchini humo kama majambazi lilishambulia kijiji cha Bakori kwa lengo la kuiba mifugo ya wakazi wa kijiji hicho.

Hata hivyo walikabiliwa vikali na wanakijiji waliojitolea kulinda usalama ambao wanaungwa mkono na serikali na kisha wakakimbilia katika msitu wa karibu. Isah amesema mbali na watu zaidi ya 40 kuuawa, wengine wengi wamejeruhiwa. 

Mauaji hayo yanaripotiwa huku Nigeria ikiendelea kusumbuliwa na ukosefu wa usalama na amani hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia harakati za majambazi, wezi wa mifugo na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Siku chache zilizopita, watu wenye silaha waliua watu wanane, akiwemo mkuu wa polisi wa kitengo na watu wengine saba katika hujuma ya hivi karibuni iliyotokea katikati mwa Nigeria. 

Jimbo la Katsina hushudiwa mauaji mara kwa mara

Wimbi la mashambulio hayo limefanyika wakati huu wa kukaribia Uchaguzi Mkuu wa Rais na Bunge, unaotazamiwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari, 2023.

Ukosefu wa usalama ni suala muhimu mno kwa wapiga kura katika nchi ambayo magenge yenye silaha yanatishia mno usalama wa wananchi hasa wa vijijini na kwenye barabara kuu ambako magenge hayo huteka nyara watu kwa ajili ya kupata vikomboleo, hasa kwenye maeneo ya kaskazini mwa Nigeria. 

Tags