Jun 17, 2016 14:44 UTC
  • Wanachama wa Boko Haram waua wanawake 18 kaskazini mwa Nigeria

Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wamewaua wanawake 18 kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hayo yamesemwa na viongozi wa kieneo walioshuhudia tukio hilo. Kwa mujibu mashuhuda, shambulio hilo lilifanywa jioni ya jana Alkhamisi katika kijiji cha Kuda jimbo la Adamawa, wakati wanawake hao walipokuwa wakishiriki msafara wa mazishi. Aidha viongozi wa kieneo wameongeza kuwa, baada ya wanachama wa Boko Haram kutekeleza hujuma hiyo, walichoma moto nyumba za wakazi wake huku wakifyatua ovyo risasi kuwalenga watu. Hii ni katika hali ambayo mkazi mmoja wa kijiji hicho amenukuliwa akisema kuwa, wanawake kadhaa wametoweka baada ya kujiri shambulizi hilo. Tayari polisi imethibitisha shambulizi hilo, ingawa idadi kamili ya watu waliopoteza maisha bado haijajulikana. Mwezi Februari mwaka huu, kijiji cha Kuda kilikumbwa pia na hujuma ya wanachama wa genge hilo la kitakfiri lililotangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, ambapo katika hujuma hiyo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Tags