Kuondoka vikosi vya Ufaransa katika nchi ya Burkina Faso
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94298-kuondoka_vikosi_vya_ufaransa_katika_nchi_ya_burkina_faso
Hatimaye vikosi vya Ufaransa vimeondoka nchini Burkina Faso na kuhitimisha uwepo wake katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika uliodumu kwa miaka 10.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2023 07:22 UTC
  • Kuondoka vikosi vya Ufaransa katika nchi ya Burkina Faso

Hatimaye vikosi vya Ufaransa vimeondoka nchini Burkina Faso na kuhitimisha uwepo wake katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika uliodumu kwa miaka 10.

Taarifa ya jeshi la Burkina Faso imeeleza kuwa, Jumapili ya juzi ilikuwa siku ya mwisho ya ushirikiano wa kijeshi baina ya mataifa hayo mawili. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kufanyika hafla ya kushusha bendera ya vikosi vya Ufaransa ambayo iliashiria kufikia tamati uwepo wa vikosi vya Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Uamuzi wa Burkina Faso wa kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa ni ushahidi wa kuzidi kuzorota uhusiano kati ya Ufaransa na koloni lake hilo la zamani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2022.

Baadhi ya mivutano hiyo inatokana na ukweli kwamba, uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Burkina Faso haujaimarisha usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na wananchi wa Burkina Faso wanaamini kwamba, ni wakoloni hao wa Ulaya ndio wanaochochea machafuko, mapinduzi ya mfululizo ya kijeshi, vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama nchini humo. 

Uhusiano wa Ufaransa na Burkina Faso ulianza kushuhudia mvutano baada ya mapinduzi ya kijeshi ya kapteni Ibrahim Traore Septemba mwaka jana (2022) ambayo yalipelekea kuondolewa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba, kuivunja serikali na kusimamisha katiba na hati ya serikali ya mpito.  Hayo yalikuwa mapinduzi ya pili ya kijeshi katika kipindi cha mwaka mmoja. Mapinduzi hayo ya kijeshi yalitokea huku viongozi wa Burkina Faso wakiituhumu Ufaransa kwamba, inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Kufuatia mzozo na mvutano huo, hatimaye Januari mwezi uliopita, serikali ya Ouagadougou ilibatilisha hati ya makubaliano ya kijeshi ya 2018 ambayo ilikuwa ikiruhusu majeshi ya Ufaransa kuweko nchini Ufaransa na ikaipatia Paris muda wa mwezi mmoja iwe imeondoa wanajeshi wake wote kutoka nchini humo.

Mataifa ya Kiafrika yanataka Ufaransa ihitimishe uwepo wake wa kijeshi katika hali ambayo, mkoloni huyo wa zamani kwa miaka mingi amekuweko barani humo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha usalama katika mataifa mbalimbali ya bara hilo hususan nchini Mali. Hata hivyo utendaji majeshi hayo katu hauungwi mkono na nchi za Kiafrika, bali mataifa hayo yanaamini kwamba, Ufaransa ikitumia kisingizio cha kupiga jeki juhudi za kurejesha amani na usalama na kupambana na ugaidi imekuwa ikitekeleza malengo ya kikoloni nyuma ya pazia.

Hafla ya kushusha bendera ya Ufaransa kuashiria kufikia tamati uhusiano wa kijeshi wa Burkina Faso na taifa hilo la Ulaya

 

Kugunduliwa kaburi la umati jirani na kambi ya jeshi ya wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali na kupenya Ufaransa katika sekta ya uchumi ya nchi za eneo katika kalibu ya kushiriki na kutoa mikopo ya muda mrefu ni ushahidi unaounga mkono wasiwasi wa mataifa haya ya Kiafrika.

Kwa mujibu wa kituo cha utafiti wa kistratejia Afrika ni kwamba, hatua ya uingiliaji wa kigeni barani Afrika imepelekea kuongezeka kwa asilimia 70 vitendo vya utumiaji mabavu vinavyohusishwa na makundi ya kigaidi katika mataifa ya eneo la Sahel Afrika. Hilo limepelekea kusajiliwa rekodi mpya ya vitendo vya kufurutu ada na utumiaji mabavu barani humo katika mwaka 2021.

Kuhusiana na hilo, hivi karibuni Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani aliyahutubu madola ya Ulaya akiyaambia: Iacheni Afrikka, acheni kuikaba koo Afrika.

Ahmad Abdallah, mweledi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Licha ya kuwa kuna ushindani na vita baina ya madola makubwa kwa ajili ya kuwa na ushawishi na udhibiti barani Afrika, lakini, vuta nikuvute ya sasa yumkini ikawa fursa kwa mataifa ya Kiafrika ili yaonyeshe kwa uhuru kamili zaidi vigezo vyao.

Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, Ufaransa licha ya kuondoka kijeshi nchini Burkina Faso haionekani kama itaondoka kikamilifu barani Afrika na kukabidhi kila kitu kwa washindani wake wa kieneo na kimataifa.