Mar 15, 2023 02:23 UTC
  • Morocco yawaonya wanaokosoa uhusiano wa nchi hiyo na Israel

Kasri ya mfalme wa Morocco imekitaka chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini humo cha PJD kiache kutoa taarifa za kukosoa na kupinga hatua ya Rabat ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na kasri ya kifalme ya Morocco imesema, jukumu la kusimamia na kutoa maamuzi kuhusu masuala ya sera za nje za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ni la Mfalme, na kwamba ofisi hiyo haitakubali kuburuzwa na kushinikiza.

Haya yanajiri siku chache baada ya chama hicho chenye mielekeo ya Kiislamu cha PJD kutoa taarifa ya kulaani matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco ya hivi karibuni, yaliyoonekana kuukingia kifua utawala haramu wa Israel, wakati huu ambapo jeshi katili la Kizayuni limeshadidisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina.

Desemba 2020, Morocco na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kwa ushawishi wa Marekani. Na kama sehemu ya makubaliano hayo, Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alikubali kutambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi. Hata hivyo serikali ya rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden imesema itauangalia upya uamuzi huo.

Mfalme wa Morocco (kulia) na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Mara kwa mara, wananchi wa Morocco wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga na kulaani hatua ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni maudhui nyeti inayogusa na kutonesha hisia za Wamorocco waliowengi ambao wanawaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, kama ilivyodhihirishwa na wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo walionyanyua bendera ya Palestina mara kadhaa wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia huko Qatar mwaka jana 2022.

Tags