Polisi wa CAR waliotekwa nyara na wabeba silaha waachiliwa huru
Mwakilishi wa mji wa Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ametangaza habari ya kuachiliwa huru polisi sita wa serikali waliokuwa wakishikiliwa na wabeba silaha nchini humo.
Amadou Aboubakar Kabirou amewambia waandishi wa habari kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika mazungumzo ya simu yaliyodumu kwa siku tatu kati ya serikali na watekaji nyara hao. Polisi hao walitekwa nyara siku Jumamosi iliyopita katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha wasiojulikana kwenye moja ya maeneo ya mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui. Duru za serikali zimetangaza kuwa, Jumatatu iliyopita watekaji nyara walipanga njama za kufanya shambulio jingine dhidi ya kituo cha polisi mjini Bangui, hata hivyo polisi wa serikali kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa walifanikiwa kuzima hujuma hiyo. Hii ni katika hali ambayo, duru za hospitali zimetangaza habari ya kuuawa watu 16 katika shambulio la watu wenye silaha mjini Bangui. Jumanne iliyopita pia, askari wa kofia ya buluu walitoa taarifa kwamba washambuliaji watu waliuawa na wengine watatu kutiwa mbaroni, huku askari mmoja wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa akijeruhiwa vibaya.