Kiongozi Muadhamu asalisha Sala ya Maiti ya Ismail Haniyeh na mlinzi wake + VIDEO na PICHA
(last modified 2024-08-01T06:43:56+00:00 )
Aug 01, 2024 06:43 UTC

Mapema leo Alkhamisi asubuhi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesalisha umati mkubwa wa Waislamu waliojitokeza katika Sala ya Maiti ya Mkuu wa Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS Ismail Haniyeh na mlinzi wake. Sala hiyo ya Maiti imesaliwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran.

Tovuti ya habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mapema leo Alkhamisi asubuhi, Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameelekea kwenye viwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran na kuongoza Sala ya Maiti ya shahid Ismail Haniyeh, mwanajihadi shujaa wa kambi ya muqawama raia wa Palestina.

Baada ya Sala hiyo, kumefanyika shughuli ya maziko kutoka kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran na kuelekea katika Medani ya Azadi yaani Medani ya Uhuru na Ukombozi, hapa Tehran. Kamanda huyo shujaa wa Palestina atazikwa mjini Doha, Qatar.

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza siku tatu za maombolezo nchini kote kufuatia kuuawa shahidi Kamanda Mwanajihadi, Ismail Haniyeh.

Taarifa ya serikali ya Iran imesema kuwa, kuuawa shahidi Ismail Haniya, Kamanda Mwanajihadi na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kumeutia majonzi Umma wa Kiislamu, wafuasi wa njia ya fikra ya Muqawama na watetezi wa ukombozi kote duniani na kuongeza kuwa, mauaji ya kiongozi huyo yameongeza ukurasa mwingine wa faili chafu na la kuaibisha la jinai zinazofanywa na tapo la kihalifu na ghasibu la Kizayuni. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (kulia) akimpokea kwa bashasha kubwa shahid Ismail Haniyeh

 

Picha kubwa na shahid Ismail Haniye katika moja ya mitaa ya Tehran
Maandamano ya wananchi wa Iran ya kulaani jinai za Israel
Sehemu nyingine ya maandamano ya wananchi wa Iran ya kulaani jinai za Israel hasa kumuua shahidi Ismail Haniyeh
Waandamanaji nchini Iran wakiwa wamenyanyua juu bendera ya shahid Ismail Haniyeh
Maandamano ya wananchi wa Iran ya kulaani jinai za Israel
Kutokana na imani yao thabiti ya kidini, wananchi wa Iran wanaipenda sana Palestina
Sehemu nyingine ya maandamano ya wananchi wa Iran ya kulaani jinai za Israel

 

Tags