Iran yatoa mkono wa pole kufuatia vifo vya wananchi wa Sudan katika mafuriko + Video
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa mafuriko nchini Sudan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Nasser Kanani, ameelezea kusikitishwa na maafa ya mafuriko katika jimbo la Port Sudan lililoko karibuni na Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu) kufuatia kuvunjika bwawa la Arba'at na kupoteza maisha makumi ya raia wa Sudan na kutoweka wengine wengi.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameliombea dua taifa la Sudan na kueleza matumaini yake kuwa nchi hiyo na wananchi wake, karibuni hivi watavuuka salama kwenye kipindi hiki kigumu na kushuhudia ustawi, utulivu na usalama katika nchi hiyo rafiki na ndugu mzuri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mvua za msimu zimesababisha kupasuka kingo za bwawa la Arba'at ambalo ndilo chanzo kikuu cha maji ya kunywa kwa wakazi wa mji wa bandari ya Port Sudan, na kupelekea vijiji 15 kukombwa na maji na kuzama kabisa na vijiji vingine 30 kuharibiwa.
Kwa mujibu wa Press TV, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na maafa hayo wamefikia 132. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Sudan.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, karibu nyumba 12,420 zimeharibiwa kikamilifu, nyumba 11,472 zimeharibiwa kwa kiasi fulani na mashamba na miundo mbinu mingi imepata hasara kubwa kutokana na mafuriko hayo.