Ulimwengu wa Spoti, Okt 6
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
Soka ya Vipofu: Iran yaibuka ya 2
Timu ya taifa ya soka ya wenye matatizo ya kuona ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika fainali za IBSA Blind Football Nations Cup 2025. Hii ni baada ya kukubali kushindwa kwa bao 1-0 na Uingereza katika mchuano wa fainali uliopigwa siku ya Jumatano. Azeem Amir alifunga bao la ushindi katika dakika za lala salama. Timu hiyo ya Iran ilianza kampeni kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Poland lakini wakatoka sare tasa dhidi ya Uingereza.

Iran pia iliichabanga India (3-0) na Korea Kusini (3-0), na Italia (1-0) kabla ya kutinga fainali. Mashindano hayo ya dunia yalifanyika katika Kituo cha Michezo cha United, Kakkanad, huko Kochi, India kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 1. Mashindano haya yalikuwa rasmi kwa nchi sita bora katika viwango vya IBSA vilivyotangazwa Januari 2025. Lilikuwa tukio rasmi la kwanza katika mzunguko mpya kuelekea duru ijayo ya Michezo ya Walemavu itakayofanyika huko Los Angeles, Marekani.
Timu ya voliboli ya wanawake ya Iran yatwaa ubingwa wa CAVA 2025
Timu ya voliboli ya wanawake ya Iran iliigaraza Uzbekistan kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji ya Wanawake wa Asia ya Kati (CAVA) jana Jumapili na kushinda taji hilo la kieneo kwa mara ya kwanza katika historia. Timu hiyo ya taifa ya Iran ya voliboli ya wanawake iliishinda Uzbekistan kwa seti za moja kwa moja za (25-14, 25-14, 25-19) katika mpambano huo wa fainali uliopigwa jana huko Tashkent, mji mkuu wa Uzbekistan. Kabla ya hapo, timu hiyo ya voliboli ya wanawake ya Iran siku ya Ijumaa iliinyoa kwa chupa mwenyeji Uzbekistan katika duru ya awali ya mashindano hayo, gazeti la Tehran Times limeripoti.

Timu hiyo ya voliboli ya wanawake ya Iran iliishinda Uzbekistan kwa seti 3-0 (25-15, 25-14, 25-16) kwenye pambano hilo la Ijumaa. Kikosi hicho kinachonolewa na mkufunzi Lee Do-hee hapo awali kilizishinda Kyrgyzstan na Tajikistan katika michuano hiyo ya kikanda ya CAVA. Iran ilianza kampeni yake huko Tashkent kwa ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Kyrgyzstan na kisha kuishinda Tajikistan kwa matokeo sawia. Kombe la Chalenji ya Voliboli ya Wanawake ya CAVA ni mashindano ya kieneo ya voliboli kwa timu za kitaifa za wanawake ambazo ni wanachama wa Chama cha Voliboli cha Asia ya Kati, ikiwa ni bodi inayosimamia mchezo huo katika eneo la Asia ya Kati na Kusini.
Michezo ya Walemavu: Iran yavuna medali lukuki India
Wanamichezo wa Iran wameendelea kung'ara na kuvuna medali kochokocho katika mashindano ya kimataifa ya walemavu yanayoendelea nchini India. Siku ya Jumamosi, Yasin Khosravi aliishindia Jamhuriya Kiislamu medali ya dhahabu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia ya 2025. Hii ni baada ya kuibuka kidedea kwenye Fainali ya Wanaume ya mchezo wa kurusha tufe (Shot Put), safu ya F57 kwa kutupa umbali wa mita 16.60 na pia akaboresha rekodi yake ya dunia. Mwanariadha wa India Soman Rana alitwaa medali ya fedha kwa kurusha umbali wa mita 14.69, huku medali ya shaba ikimwendea Teijo Koopikka wa Finland kwa kutupa umbali wa mita 14.51.

Wairani Aliasghar Javanmardi kwenye mchezo wa kurusha kisahani (Discus) kwa Wanaume kitengo cha F11, Amirhossein Alipour kwenye Risasi za Wanaume F11, Elham Salehi kwenye Kurusha Mkuki wa kwa Wanawake kategoria ya F54, Saeid Afrooz kwenye Mkuki kwa Wanaume wa safu ya F34, Hassan Bajoulvand kwenye safu ya Wanaume kurusha kisahani kategoria ya F54 hapo awali walishinda medali sita za dhahabu na kuongezea idadi ya medali za dhahabu ya Iran. Kama hilo halitoshi, Ali Baziyar wa Iran alijishindia medali ya dhahabu katika siku ya Jumamosi kwenye mashindano hayo ya kimataifa, kwenye Fainali ya Kurusha Mkuki F54 kwa Wanaume kwa kurusha umbali wa mita 32.24. Zaidi ya wanariadha 2,000 kutoka nchi 104 wanapambania medali 186 - wanaume 101, wanawake 84.
Singida wapokewa kifalme
Klabu ya soka ya Singida Black Stars ya Tanzania imepokewa kifalme katikak Uwanja wa Bombadia huko Singida Mjini, waliporejea mkoani humo baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alhilal ya Sudan katika mechi ya fainali iliyopigwa Septemba 15. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Singida kutwaa taji hilo la kieneo. Mkufunzi wa klabu hiyo, Migeul Gamondi amesema wachezaji wake hawapasi kubweteka kwa kutwaa taji hilo, kwani wangali wana kibarua kinawasubiri mbele yao. Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ni mmoja wa shakhsia watajika waliokuwepo katika Uwanja wa Bombadia Singida Mjini katika shamrashamra za kusherehekeka ubingwa wa Singida, ambapo yeye ni mlezi wa klabu hiyo ya soka.
Dondoo za Michezo na Palestina
Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran Ahmad Donyamali amewataka wenzao katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuunda msimamo mmoja dhidi ya utawala wa Israel na kuusaidia kuupiga marufuku michezo ya kimataifa. Katika barua kwa mawaziri wa michezo wa nchi 57 wanachama wa OIC, Donyamali alisema kuna haja ya kuunda "Unified Islamic Sports Front" ili kuitaka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kusimamisha uwepo wa utawala wa Israel katika michezo ya kimataifa. Amesema katika barua hiyo kwamba utawala ghasibu wa Israel umehujumu pakubwa Mkataba wa Olimpiki na moyo wa kweli wa michezo kupitia hatua zake katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu katika kipindi cha miongo minane iliyopita, na hasa tangu Oktoba 2023, ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Ubaguzi wa Rangi katika Michezo (uliopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1985) unathibitisha wazi kwamba michezo haipaswi kuwa jukwaa la kuhalalisha tawala zilizoanzishwa kwa ubaguzi na ukandamizaji.

Donyamali amesema nchi wanachama wa OIC zinapaswa kutaka rasmi kusimamishwa na kufukuzwa Israel katika mashindano ya kimataifa ya michezo. Huku hayo yakiarifiwa, Kocha Mkuu wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, Pep Guardiola, katika ujumbe wake wa video, aliwataka watu wa Uhispania kujitokeza katika mitaa ya Barcelona Jumamosi mchana ili kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza na kupinga mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni. Aidha amezitaka serikali kote duniani kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kukomesha mauaji hayo ya kimbari na kuzitaka zitumie mashinikizo makali ya kisiasa na kidiplomasia dhidi ya utawala wa Kizayuni. Mkufunzi huyo wa Man City amesema. Kocha huyo wa timu ya soka ya Manchester City amewahi kukosoa vikali ukimya wa walimwengu kuhusiana na jinai za utawala wa kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Ubinadamu umetoweka."

Hii ni katika hali ambayo, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino amesema, taasisi hiyo haiwezi kutatua ‘masuala ya kijiopolitiki’, licha ya kuendelea kuandamwa na mashinikizo kimataifa ya kuitaka isimamishe uanachama wa Israel kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari unayoendelea kufanya utawala huo wa kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, ambayo hadi sasa yameshateketeza roho za watu zaidi ya 65,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Kupitia taarifa aliyotoa siku ya Alkhamisi, Infantino "amegusia umuhimu wa kuimarishwa amani na umoja kwa muktadha wa kinachoendelea huko Gaza.” "Kama FIFA, tunatumia mchezo wa soka kuwaleta watu pamoja," amedai Infantino na kuendelea kusema: "fikra zetu zipo kwa wale wanaoendelea kuteseka maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na machafuko, lakini kwa sasa ujumbe mahususi ni umoja na amani." Ikumbukwe kuwa, mnamo mwaka 2022, shirikisho hilo la soka duniani liliifungia Russia kushiriki mashindano ya kombe la dunia la soka yaliyofanyika nchini Qatar baada ya kuanzisha vita dhidi ya Ukraine, lakini hadi sasa imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya Israel. Haya yanjiri huku Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran likilitoa wito wa kutimuliwa Israel katika soka kutokana na mauaji yake ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Shirikisho la Soka la Iran amesema kuwa, wameliandikia Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mara kadhaa wakitaka kusimamishwa kwa Shirikisho la utawala wa kizayuni wa Israel. Amir Mehdi Alavi, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Shirikisho la Kandanda la Iran amebainisha kuwa, Shirikisho la Soka la Iran limetuma barua mara kadhaa kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) likitaka kusimamishwa uanachama wa shirikisho la soka la utawala wa kizayuni wa Israel kutokana utawala huo ghasibu kutekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Palestina zaidi ya wanamichezo 800 wameuawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 2023.
Na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kujenga Kijiji cha AFCON jijini Arusha ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Akizungumza Oktoba 2, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Dkt. Samia alisema ujenzi wa kijiji hicho ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kushirikiana na nchi nyingine kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
…………………MWISHO………………