Raisi: Maadui wameshindwa kuwakatisha tamaa wananchi wa Iran
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema adui amefeli katika njama zake za kuitenga Jamhuri ya Kiislamu na dunia, na pia kuwakatisha tamaa wananchi wa nchi hii.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari leo Jumanne hapa mjini Tehran, Rais Raisi ameashiria mafanikio ya serikali yake ya kuimarisha uhusiano wa kigeni na kusisitiza kuwa, sera hiyo ndio msingi wa kugonga ukuta njama za maadui dhidi ya taifa hili.
Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa: Tumefuatilia kuimarisha uhusiano na majirani, na tumefanikiwa katika uwanja huo. Aidha kuhuisha uhusiano na nchi za Kiislamu kumepelekea ongezeko la asilimia 14 la mabadilishano ya kibishara na mataifa jirani.
Rais wa Iran ameeleza kuwa, serikali yake imeweka rekodi mpya ya kuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi za nje, na ushirikiano huo utaimarika zaidi kwa Iran kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO na kundi la BRICS.
Kadhalika Rais Raisi amesema maadui wameshindwa kulitumbukiza taifa la Iran katika dimbwi la masononeko na kukata tamaa kupitia vita vya mitandao dhidi ya vituo vya gesi, miezi michache baada ya kuundwa baraza la mawaziri la Iran.
Kuhusu ghasia zilizochochewa na maajinabi hapa nchini mwaka jana, Sayyid Raisi amesema maadui walikusudia kukwamisha ustawi na maendeleo hapa nchini, lakini njama hizo zikafeli kutokana na kusimama kidete wananchi wa Iran.
Amesema kuondolewa vikwazo vya Marekani ni moja ya mambo yanayofuatiliwa na serikali yake, na kwamba inafuatilia pia kujumuishwa Iran katika miungano ya kieneo na kimataifa.
"Baadhi wanasema njia pekee ya kuondokana na matatizo yetu ni tabasamu la Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, lakini tunasisitiza kuwa, katu hatutasubiri matabasamu yao," ameongeza Raisi.