Iran kuunda makombora mapya ya hypersonic kuikabili Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102076-iran_kuunda_makombora_mapya_ya_hypersonic_kuikabili_israel
Kamanda wa ngazi ya juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amefichua mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunda makombora mapya ya hypersonic ambayo anasisitiza kuwa yataufanya utawala wa Kizayuni ulipe gharama kubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 10, 2023 10:38 UTC
  • Iran kuunda makombora mapya ya hypersonic kuikabili Israel

Kamanda wa ngazi ya juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amefichua mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunda makombora mapya ya hypersonic ambayo anasisitiza kuwa yataufanya utawala wa Kizayuni ulipe gharama kubwa.

Katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim, Brigedia Jenerali Abbas Nilforoushan, Naibu Kamanda wa Operesheni za SEPAH amesema teknolojia ya Iran ina uwezo wa kuboresha na kuyaongeza nguvu makombora yake yaweze kupiga hadi umbali wa kilomita 2,000.

Brigedia Jenerali Nilforoushan amesema Iran imejiwekea mipaka ya makombora yake yasipige zaidi ya kilomita 2,000, kwa mujibu wa amri ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei.

Kamanda huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua zaidi kwa kusema, "Mifumo ya ulinzi wa makombora ya utawala wa Kizayuni yamepitwa na wakati, na haiwezi kutungua kombora la Fattah."

Ikumbukwe kuwa, mwezi Juni mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua kombora lake la kwanza la balistiki la hypersonic lililopewa jina la 'Fattah'.  Kombora hilo lina uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 1,400, sambamba na kutambua na kuharibu ngao za aina zote za makombora.

Kombora la hypersonic la Fattah

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, makombora ya hypersonic yana kasi mara tano zaidi ya mwendo wa sauti, na hivyo kuyapa uwezo wa aina yake ya kutoweza kuyatungua.

Mafanikio ya viwanda vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika kuunda makombora ya balistiki katika miaka ya karibuni yanayatia tumbojoto madola ya Magharibi.