Ebrahim Raisi: Iran imethibitisha kuwa ni rafiki wa Iraq katika nyakati ngumu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102222-ebrahim_raisi_iran_imethibitisha_kuwa_ni_rafiki_wa_iraq_katika_nyakati_ngumu
Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kusita kutoa msaada wowote kwa ajili ya kuihami Iraq katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh (ISIS) na imethibitisha kivitendo kuwa ni rafiki mwaminifu wa Iraq katika nyakati ngumu.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Sep 14, 2023 07:39 UTC
  • Ebrahim Raisi: Iran imethibitisha kuwa ni rafiki wa Iraq katika nyakati ngumu

Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kusita kutoa msaada wowote kwa ajili ya kuihami Iraq katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh (ISIS) na imethibitisha kivitendo kuwa ni rafiki mwaminifu wa Iraq katika nyakati ngumu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatano jioni wakati alipoonana na Fuad Mohammed Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq aliyeko ziarani hapa Iran, na huku akishukuru ukarimu wa serikali na taifa la Iraq katika kuwahudumia mazuwari na wafanyaziara ya Imam Husain AS katika maeneo matukufu nchini Iraq amesisitiza kuwa, ushirikiano uliooneshwa na wizara za serikali ya Iraq, vikosi vya ulinzi wakiwemo pia wanamapambano wa Hashd al-Sha'abi, na vile vile juhudi za wananchi wa Iraq hasa katika kuwahudumia wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS, ni wa kupigiwa mfano, ni muhimu na ni wenye taathira kubwa.

Uhusiano wa Iran na Iraq unazidi kuimarika siku baada ya siku

Rais Raisi aidha amesema, juhudi za mashahidi wa Iran na Iraq, akiwemo Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na Abu Mahdi Al-Muhandis aliyekuwa naibu wa mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la Hashd al Sha'abi waliouliwa kidhulma na Wamarekani nchini Iraq, pamoja na uhusiano wa kidini, kiutamaduni na kihistoria baina ya mataifa haya mawili ni katika mambo ya kujivunia na yanatoa fursa nzuri ya kuwepo ushirikiano zaidi baina ya nchi hizi mbili ndugu za Kiislamu. 

Kwa upande wake, Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kwenye mazungumzo hayo kwamba, kwa kuzingatia mikutano inayoendelea ya wajumbe wa kidiplomasia na maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili za Iran na Iraq, tutaona kuwa uhusiano wa nchi hizi ndugu ni imara na unaozidi kustawi na kwamba nchi yake imejitolea kikamilifu kutekeleza makubaliano yanayofikiwa.