Iran: Tutatoa jibu madhubuti kwa vitisho vya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102266-iran_tutatoa_jibu_madhubuti_kwa_vitisho_vya_israel
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu madhubuti kwa vitisho vyovyote na vitendo haramu vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2023 08:25 UTC
  • Iran: Tutatoa jibu madhubuti kwa vitisho vya Israel

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu madhubuti kwa vitisho vyovyote na vitendo haramu vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa hili.

Amir Saeid Iravani amesema hayo katika barua aliyomuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo, Ferit Hoxha.

Ameeleza bayana kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba haitasita kutekeleza haki zake halali za kulinda usalama na maslahi yake ya kitaifa, sanjari na kuwadhaminia usalama wananchi wake." 

Kauli hii imekuja chini ya wiki moja baada ya David Barnea, Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) kutoa vitisho kuwa Israel itawaua makamanda wa ngazi za juu wa Iran katikati ya Tehran.

Barnea alidai kuwa, Mossad imezima majaribio 27 ya mashambulizi dhidi ya Israel katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, eti yaliyopanga na kuratibiwa na Iran.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha tuhuma hizo za mkuu wa Mossad dhidi ya Iran na kueleza kuwa, madai hayo hewa hayana mashiko wala msingi wowote.

David Barnea, Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad)

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, bwabwaja hizo za Mkurugenzi wa Mossad ni muendelezo wa ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Israel dhidi ya taifa la Iran.

Amesema utawala wa Kizayuni unatoa madai ya namna hiyo kujaribu kuhalalisha vitendo vyake haramu na vinavyokanyaga sheria za kimataifa dhidi ya mataifa mengine duniani, kama vile Palestina.