Oct 23, 2023 03:02 UTC
  • Rais Raisi: Hakuna matumaini tena kwa Baraza la Usalama la UN kutekeleza jukumu la kulinda amani ya dunia

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini kuwa, hakuna matumaini tena kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lake la kulinda amani ya dunia.

Katika mazungumzo hayo na Bi Naledi Pandor, Seyed Ebrahim Raisi, amepongeza juhudi na ufuatiliaji uliofanywa na Afrika Kusini katika kufanikisha uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS na akasema, kujihisi serikali na wananchi wa Afrika Kusini kuwa wana jukumuu la kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kuonyesha chuki na kuchukizwa kwao na dhulma zinazofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni ni jambo lenye thamani na linalostahiki kupongezwa.
 
Kwa mujibu wa IRNA, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehoji utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Wakati Marekani inapokuwa mshirika wa jinai dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza kwa kutuma zana na silaha kwa utawala wa Kizayuni, na kuzuia pia kupitishwa azimio la kulaani jinai hizo katika Baraza la Usalama, hakuwi na matumaini tena kwa baraza hilo kutekeleza jukumu la kulinda na kudumisha amani ya dunia.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Raisi ameashiria jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi hususan wanawake na watoto wa Kipalestina na akauelezea msimamo wa Afrika Kusini wa kuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel usipate hadhi ya mwanachama msikilizaji katika Umoja wa Afrika kuwa ni hatua ya uwajibikaji pia.

 
Katika mazungumzo hayo, Naledi Pandor amesema, uanachama wa Iran katika BRICS uliafikiwa na nchi zote wanachama na akasisitiza kuwa, Iran inaweza kutoa mchango athirifu katika kuinua hadhi ya BRICS na katika utekelezaji wa juhudi za pamoja za nchi wanachama kwa ajili ya kupatikana ustawi wa kiuadilifu.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Bi Naledi Pandor aliwasili Tehran jana Jumapili akiongoza ujumbe maalumu wa nchi yake, na akakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian.../

 

Tags