Raisi: Kulaaniwa Israel katika Baraza Kuu la UN ni mafanikio muhimu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104104-raisi_kulaaniwa_israel_katika_baraza_kuu_la_un_ni_mafanikio_muhimu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya hivi karibuni ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio juu ya vita vya Gaza ni mafanikio muhimu katika mkondo wa kusitisha jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2023 23:30 UTC
  • Raisi: Kulaaniwa Israel katika Baraza Kuu la UN ni mafanikio muhimu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya hivi karibuni ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio juu ya vita vya Gaza ni mafanikio muhimu katika mkondo wa kusitisha jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Rais Ebrahim Raisi aliyasema hayo jana Jumapili katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa, "Kura ya ndio ya (aghalabu ya nchi wanachama) kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika la kulaani jinai za Israel (dhidi ya Wapalestina wa Gaza) licha ya vitisho na ahadi za mfumo wa ubeberu, ni mafanikio muhimu."

Huku akitoa mwito wa kufanyika kikao cha dharura cha viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kujadili njia za kuwanusuru Wapalestina wa Gaza, Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, suala la Palestina daima linapaswa kuzingatiwa kuwa ni suala muhimu zaidi na kero kubwa ya nchi zote za Kiislamu.

Amesema utawala wa Kizayuni ambao ni mashine ya vita, licha ya uungaji mkono wa kisiasa, kiusalama na wa vyombo vya habari wa Marekani, umeshindwa kurejesha fahari yake iliyotoweka, huku wanamapambano wa Palestina na mrengo wa muqawama ukipata mafanikio makubwa katika medani ya vita.

Jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Kabla ya hapo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliiambia televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kuwa: Jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni za kuwaua wanawake na watoto kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani na nchi kadhaa za Ulaya, zimewashtua na kuwakasirisha watu wengi duniani dhidi ya utawala huo ghasibu, kwa namna ambayo tunaweza kusema watu wa dunia, wataalamu na wanasiasa wengi wako upande mmoja, na utawala wa Marekani, nchi kadhaa za Ulaya na utawala bandia wa Israel wako upande mwingine.

Mashambulizi ya Wazayuni yaliyoanza tokea Oktoba 7 hadi sasa yameuwa shahidi zaidi ya watu elfu 8, kujeruhi karibu elfu 20 na kuharibu sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza.

Ijumaa iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha rasimu ya azimio lililopendekezwa na nchi za Kiarabu na kutaka kutekelezwa usitishaji vita wa kibinadamu haraka iwezekanavyo huko Gaza. Azimio hilo lilipasishwa kwa kura 120 za ndio mkabala wa 14 za hapana, huku nchi 45 zikijizuia kupiga kura. Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani zililipigia azimio hilo kura ya hapana.