Rais wa Iran: Hakuna nchi yenye ujasiri wa kuishambulia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104852-rais_wa_iran_hakuna_nchi_yenye_ujasiri_wa_kuishambulia_iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Iran imefikia kiwango cha kujitosheleza katika sekta ya kijeshi na hakuna nchi inayoweza kuthubutu kuivamia ardhi ya nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 16, 2023 08:10 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raisi
    Sayyid Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Iran imefikia kiwango cha kujitosheleza katika sekta ya kijeshi na hakuna nchi inayoweza kuthubutu kuivamia ardhi ya nchi hii.

Sayyid Ebrahim Raisi ameyasema hayo leo katika mjumuiko mkubwa wa wananchi wa Shahr-e Kord huko Kusini Magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu inatokana na uungaji mkono na mahudhurio ya wananchi katika nyanja zote. Amesema: Uungaji mkono wa wananchi umewapa nguvu viongozi na kuwafanya wazungumze bila ya kigugumizi chochote katika kutangaza misimamo ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Iran inasimama kidete dhidi ya mfumo wa kibeberu na kusema: "Kama ambavyo kuwepo viwanda vya zana za kijeshi na vikosi vya jeshi ni chanzo cha nguvu kwa nchi, vilevile nguvu za kiuchumi, sayansi na teknolojia, maarifa, damu ya mashahidi na uungaji mkono wa wananchi pia vinaimarisha nguvu ya nchi yetu." 

Gaza, Palestina

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameeleza masikitiko yake kutokana na dhulma ambayo inaendelea kufanywa hivi sasa na utawala wa kibeberu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusema: "Katika siku hizi watu wote wa Iran, Umma wa Kiislamu na jamii ya binadamu wako kwenye majonzi kwa ajili ya watu wa Palestina, na wanadamu wote wanatangaza hasira na kuchukizwa kwao na mfumo wa ubeberu, Wamarekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake huko Magharibi na Ulaya.