Zarif: Iran haitopumzika hadi ugaidi utokomezwe duniani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema katu haitapumzika hadi pale ugaidi na idiologia za kuchupa mipaka za magaidi zitakapotokomezwa kikamilifu.
Akitoa radiamali yake juu ya mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni kama ya Istanbul, Dhaka na Baghdad yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu, Muhammad Javaz Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameitaka jamii ya kimataifa kuiga mfano wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutokata tamaa katika vita dhidi ya ugaidi. Zarif ametuma taarifa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter na kusema: "Hatupaswi kupumzika hadi tuhakikishe wale wote waliohusika na mashambulizi ya kigaidi ya Istanbul, Dhaka na Baghdad wanatokomezwa sambamba na misimamo yao ya kufurutu ada." Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea jana mjini Baghdad nchini Iraq na kuua zaidi ya watu 170 na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuisadia serikali na taifa la Iraq hadi pale magaidi watakapoangamizwa kikamilifu nchini humo. Mbali na mashambulizi ya Baghdad, Julai Mosi genge la kigaidi lenye mafungamano na Daesh lilitekeleza hujuma ya kigaidi katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka na kuua raia zaidi 20, siku tatu baada ya magaidi hao wakufurishaji kuua watu 45 katika hujuma ya kigaidi katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul nchini Uturuki.