Jan 10, 2024 02:42 UTC
  • Indhari ya balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa kwa Marekani kuhusu vitendo vya kichochezi

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha madai ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu Bahari Nyekundu na kuonya dhidi ya hatua zozote za uchochezi zinazofanywa na Wamarekani.

Jumatatu ya tarehe 8 Januari, Amir Saeid Iravani, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alimuandika barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, ambaye anashikilia urais wa zamu wa Baraza la Usalama ambapo sambamba na kulaani kwa uwazi madai yasiyo na msingi yaliyotolewa katika mkutano huo amebainisha kwamba, tuhuma hizo, hazina msingi wowote.

Iravani ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiupa umuhimu mkubwa usalama wa baharini na uhuru wa usafiri wa baharini na inasisitiza dhamira yake isiyoyumba ya kushikamana na majukumu yake ya kimataifa na kudumisha amani na usalama katika eneo.

Chris Lu, naibu balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama, bila kutaja sababu halisi za mashambulizi katika Bahari Nyekundu, alisema, mashambulizi haya hayakubaliki na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Aidha amesema kuwa, Mashambulio ya Wayemen dhidi ya meli za kimataifa yamefikia hatua nyeti sana.

Chris Lu, naibu balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa

 

Madai ya afisa huyo wa Marekani yanatolewa katika hali ambayo, jeshi la Yemen liliingilia kati na kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kusimamisha baadhi ya meli katika Bahari Nyekundu na Lango-Bahari la Bab al-Mandab katika siku za hivi karibuni na kuonya kuwa, hawataruhusu meli hizo kuuita na kuelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel). Hatua hiyo ya jeshi la Yemen inaonyesha kuwa, kinyume na madai ya maafisa wa Marekani, nchi na mamlaka huru za eneo hili hazivumilii uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo na wanataka kusitishwa uingiliaji wa Washington katika masuala ya mataifa mengine.

Katika upande mwingine, hatua za serikali ya Marekani katika kuunda muungano wa wanamaji katika Bahari Nyekundu ni ishara tosha ya hatua za Washington zinazokiuka sheria za kimataifa. Siasa za uingiliaji kati za Marekani katika eneo hili hazina kikomo, na maafisa wa Washington wametangaza kuunda muungano wa wanamaji katika Bahari Nyekundu na washirika wao wa Magharibi katika siku za hivi karibuni, wakati nchi za Magharibi na washirika wa kawaida wa Ikulu ya White House, zikiwemo Ufaransa, Uhispania na Italia zimejiondoa kwenye muungano huo.

Vikosi vya wananchi katika eneo katika miezi ya hivi karibuni na hasa baada ya kuanza operesheni za makundi ya muqawama wa Palestina huko Gaza, yamesimama wazi dhidi ya hatua za uingiliaji kati za Marekani na hayaruhusu wanajeshi wa Marekani kuendeleza mivutano yao nchini Iraq, Lebanon na Bahari ya Sham.

Operesheni ya wanamaji wa Yemen

 

Hatua za jeshi la Yemen pia zinaonyesha kuwa, kinyume na misimamo ya vitisho ya viongozi wa Marekani, Jeshi la Wanamaji la Marekani haliwezi kukabiliana na majibu na mashambulizi ya jeshi la wanamaji wa jeshi la Yemen.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia misingi ya siasa zake za nje imekuwa ikisisitiza kila mara ulazima wa kuondolewa askari wa kigeni katika eneo hili na kwamba, kuendelea kuwepo askari hao ni kuzidisha matatizo na ukosefu wa usalama. Serikali za kikanda pia, ikiwa ni pamoja na Iraq na Syria, zimesisitiza mwisho wa uwepo wa kijeshi wa Marekani.

Matukio mapya katika eneo hili na nafasi ya vikosi vya muqawama na vya wananchi kwa ajili ya kuondoka vikosi vya kigeni na kukabiliana na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya mataifa mengine kwa namna fulani inaakisi hisia ya uhuru na chuki dhidi ya uingiliaji kati ambao umekuwa  na nafasi kubwa katika kuzusha migogoro na matatizo katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Tags