Mar 26, 2024 11:42 UTC
  • Ismail Haniya wa Hamas afika Tehran, akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Ismail Haniyah, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), leo amewasili Tehran na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian ambapo wamejadili matukio ya hivi karibuni katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa IRNA, wawili hao wamejadili masuala kadhaa ya kieneo hasa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na hali kadhalika hali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita tangu utawala haramu wa Israel uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia uwezo wake wote wa kidiplomasia kushinikiza usitishwaji vita na kutumwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.

Safari ya Haniyah mjini Tehran imefanyika siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu haja ya kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza.

Wapalestina elfu 32,333 wameuawa shahidi na wengine elfu 74,694 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la utawala haramu wa Israel katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023. Aghalabu ya waathirika wa jinai za Israel huko Gaza ni wanawake na watoto.

Baada ya operesheni ya kimbunga ya Al-Aqsa na kushadidi mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemtembelea Haniyah mara kadhaa huko Doha, Qatar na kujadiliana naye kwa karibu kuhusiana na matukio hayo.

 

Tags