Apr 11, 2024 07:55 UTC
  • Amir-Abdollahian: Israel imeongeza kasi ya kuporomoka kwake kwa kuwaua watoto na wajukuu wa kiongozi wa HAMAS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema mauaji ya hivi karibuni yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wanafamilia wa kiongozi wa Hamas yanaongeza kasi ya kuporomoka kusio na shaka kwa utawala huo.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika ujumbe aliomwandikia Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, hapo jana.
 
Mapema jana hiyohiyo, watoto watatu na wajukuu watatu wa kiongozi huyo mkuu wa Hamas waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi la anga la Israel lililolenga gari katika kambi ya wakimbizi ya al-Shat kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza, unaohimili vita vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.
Watoto wa Kiongozi wa Hamas waliouliwa na jeshi la kigaidi la Kizayuni

Amir-Abdollahian amelaani ukatili huo na kuutaja kuwa ni shambulio la jinai na la woga la utawala ghasibu wa Kizayuni.

Amesema, kuuawa shahidi wanafamilia wa kiongozi wa Hamas "ni kitangulizi cha msaada na auni ya Mwenyezi Mungu na ushindi kwa taifa la Palestina, na chanzo cha fedheha ya milele, kushindwa, fedheha kwa Wazayuni wahalifu na waungaji mkono wao".

Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa Kiongozi wa Hamas umetamatika kwa kueleza kwamba, matukio hayo ya kujitolea mhanga "bila shaka yataongeza imani thabiti ya taifa la Palestina na azma ya [kutumia] uthabiti na muqawama kuelekea ukombozi wa Palestina inayopendwa na yataharakisha kushindwa na kuporomoka kusikoepukika kwa utawala usio na msingi wa Kizayuni". 

Awali kabla ya hapo, Rais Ebrahim Raeisi alikuwa amemtumia Haniya ujumbe sawa na huo, akilitaja shambulio hilo la Israel kuwa ni ishara nyingine ya ukatili wa Tel Aviv.../

 

Tags