Apr 17, 2024 11:41 UTC
  • Kujitetea kwerevu kwa Iran kwa ajili ya Gaza

Hatua ya Iran kujitetea kihalali dhidi ya shambulio la kichokozi la utawala wa Kizayuni katika ubalozi mdogo wake nchini Syria, ambayo ilifanyika kwa utaratibu wa hali ya juu na kupitia silaha tofauti za mashambulio, imekuwa na athari na matokeo ya kieneo na kimataifa angalau imepelekea wakaazi wa Gaza kupata usiku mmoja wa amani na utulivu.

Kwa muda wa miezi sita mfululizo eneo la Gaza limekabiliwa na mashambulizi ya makombora na mabomu ya jeshi la utawala wa Kizayuni na silaha nyingine ambazo unapewa na nchi za Magharibi hususan Marekani. Kwa kuzingatia kiwango cha mashambulizi hayo ambayo hadi sasa yamepelekea kuuawa shahidi  na kujeruhiwa zaidi ya Wapalestina laki moja na wengine milioni moja na nusu kuhama makazi yao pamoja na uharibifu wa maelfu ya majengo ya raia, matibabu na miundo mbinu ya eneo hilo, kushuhudia usiku mmoja wa amani wakaazi wa Gaza pia kumevutia hisia za waandishi wa vyombo vya habari na katika siku chache zilizopita suala hilo limepewa umuhimu maalumu na vyombo vya habari.

Licha ya kuwa viongozi wa nchi nyingi wameikumbusha Israel na waitifaki wake kwamba, lau utawala wa Kizayuni haungetekeleza mauaji ya umwagaji damu huko Gaza au kushambulia ubalozi mdogo wa Iran ambao unahesabiwa kuwa sehemu ya ardhi yake kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa, Iran haingelazimika kuacha subira yake ya kimkakati na kuchukua hatua ya moja kwa moja na ya pande zote kwa ajili ya kujitetea. Hata hivyo, utawala wa Kizayuni pamoja na kupuuza matakwa hayo, umeanzisha tena mashambulizi yake dhidi ya Gaza na kuitishia Iran kwa mashambulizi mapya, na kwa njia hiyo, kuvuruga fursa mpya zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kuanza usitishaji vita huko Gaza na vilevile kupunguza mizozo na mivutano na hivyo kupelekea eneo kukumbwa tena na hali ya utata na wasiwsi.

Sehemu ya droni za Iran

Hii ina maana kwamba dhima ya matokeo ya kuanza tena uvamizi huko Gaza au mashambulizi mpya dhidi ya Iran utaibeba utawala wa Kizayuni, kwa sababu maafisa wakuu wa kijeshi wa Iran wametangaza wazi kuwa suala hilo limemalizika kwa mtazamo wa Iran, isipokuwa pale Israel itakapoanzisha tena uchokozi mwingine, ambapo jibu la Iran mara hii litakuwa kali zaidi kuliko la hapo awali. Wakati huohuo na kwa kuzingatia misimamo iliyotangazwa na waitifaki wa Israel, hususan Marekani, hakuna mtu atakayeweza kuiokoa Tel Aviv katika jibu kali na mashambulizi ya pande zote ya Iran.

Serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu ilidhani kuwa kwa kutekeleza sera za maangamizi na mauaji ya umwagaji damu huko Gaza, ingeweza kuhamisha idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo hadi Misri na nchi zinginezo na kuitenga kabisa Gaza na Hamas lakini kiutendaji sera hiyo ilikuwa jinai nyingine yake ya kivita na zimeongeza kesi nyingine mbili kwenye kesi za awali za Netanyahu.

Moja ni utekelezaji wa jinai za kivita na mauaji ya halaiki huko Gaza, na pili ni kushindwa kuokoa maisha ya mateka wa Israel na kuuliwa baadhi yao na jeshi la Israel yenyewe.

Serikali ya Netanyahu inayopinga amani na ya kichokozi ilidhani kwamba kushambulia ubalozi mdogo wa Iran kungekuwa kwa maslahi yake, lakini hivi sasa kumekuwa dhidi yake na kupelekea kupungua kila siku satwa yake. Ni wazi kuwa iwapo atakosea tena kimahesabu bila shaka atakuwa amefanya kosa jingine kubwa ambalo mara hii litamuangamiza kabisa kisiasa.

Tags