Iran yaionya Israel dhidi ya 'chokochoko mpya' kuhusu Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i114570-iran_yaionya_israel_dhidi_ya_'chokochoko_mpya'_kuhusu_lebanon
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametahadharisha kuhusu chokochoko yoyote mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa Lebanon.
(last modified 2024-07-28T07:27:05+00:00 )
Jul 28, 2024 07:27 UTC
  • Nasser Kan'ani
    Nasser Kan'ani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametahadharisha kuhusu chokochoko yoyote mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa Lebanon.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani, ameyasema hayo leo Jumapili akiashiria taarifa iliyotolewa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon na misimamo ya baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya kukanusha kuhusika na shambulio la Majdal Shams katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Golan la Syria na kusema: "Utawala wa kibaguzi wa Israel, baada ya miezi kumi mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya umati ya watoto na wanawake wa Kipalestina, sasa unataka kupindisha maoni ya umma na mtazamo wa walimwengu kuhusiana na jinai zake kubwa huko Palestina kwa kutumia hadaa ya tukio la kubuni."

Kan'ani amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna ustahiki wa kimaadili wa kutoa maoni kuhusu tukio lililotokea katika eneo la Majdal Shams, na madai ya utawala huo dhidi ya wengine hayatasikilizwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekutaja kuunga mkono utulivu na usalama wa Lebanon na eneo zima la Magharibi mwa Asia dhidi ya chokochoko za utawala ghasibu wa Kizayuni kuwa ni jukumu la jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesisitiza kuwa, hatua yoyote ya kijinga ya utawala huo inaweza kutengeneza mazingira ya ukosefu wa utulivu, usalama na moto wa vita katika eneo hili, na katika hali hiyo Israel ndio itakayokuwa muhusika mkuu wa matokeo na athari zisizotarajiwa za mienendo yake ya kijinga.

Nasser Kan'ani

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameishauri serikali ya Marekani kuwajibika kimataifa na kimaadili badala ya kuupatia utawala wa Kizayuni silaha za maangamizi makubwa na kumuenzi Waziri Mkuu mtenda jinai wa utawala wa Israel, baada ya miezi kumi ya kutenda jinai dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ina iuzuiye utawala wa Kizayuni kuwasha moto mpya ambao miali yake itawazakumba Wazayuni wote.

Jeshi la utawala ghasibu wa Israel limeshambulia vijiji 5 vya mpakani vya Lebanon kwa makombora kadhaa katika mashambulizi yake mapya kusini mwa nchi hiyo.

Mashambulio hayo yamefanyika baada ya utawala wa Kizayuni kudai kuwa eneo la Majdal Shams, katika Golan linayokaliwa kwa mabavu, limeshambuliwa kwa makombora ya Hizbullah, ambapo Wazayuni 12 wameuawa na wengine 40 wamejeruhiwa.