Amoli Larijani: Uislamu hauna uhusiano na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11488-amoli_larijani_uislamu_hauna_uhusiano_na_ugaidi
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran amesema Uislamu hauna uhusiano na ugaidi na kuongeza kuwa kile kinachodaiwa kuwa ni 'Ugaidi wa Kiislamu' ni fikra ya Wamagharibi ambao wanaunga mkono kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na makundi mengine ya wakufurishaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2016 09:30 UTC
  • Amoli Larijani: Uislamu hauna uhusiano na ugaidi

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran amesema Uislamu hauna uhusiano na ugaidi na kuongeza kuwa kile kinachodaiwa kuwa ni 'Ugaidi wa Kiislamu' ni fikra ya Wamagharibi ambao wanaunga mkono kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na makundi mengine ya wakufurishaji.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mkutano wake wa kila wiki na maafisa wa ngazi za juu wa vyombo vya mahakama nchini. Ameongeza kuwa, baadhi ya serikali za Kimagharibi zinaeneza istilahi ya 'Ugaidi wa Kiislamu' na hivyo kueneza chuki dhidi ya Uislamu.

Ayatullah Amoli Larijani amebainisha masikitiko yake kufuatia hujuma ya kigaidi ya hivi karibuni nchini Ufaransa pamoja na jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi nchini Uturuki na kusema matukio hayo yamepelekea watu wasio na hatia kuuawa. Ameongeza kuwa, msimamo wa kimsingi na kimantiki wa Iran ni kulaani kila hatua ambayo inaenda kinyume na uthabiti, usalama na utulivu wa nchi na serikali zilizochaguliwa na wananchi.

Ayatullah Amoli Larijani pia amesema makosa ambayo yamefanywa na watawala wa hivi sasa wa Uturuki ni kuwa rafiki na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuhasimiana na Syria nchi ambayo iko katika mhimili wa muqawama au mapambano dhidi ya Wazayuni.

Kuhusu hujuma ya kigaidi ya Nice, Ufaransa, Amoli Larijani amesisistiza kuwa, hakuna 'gaidi mzuri na gaidi mbaya' na kuongeza kuwa kitendo chochote cha kigaidi popote pale kinapotokea duniani ni kibaya lakini kwamba serikali za Magharibi hazina azma imara ya kukabiliana na ugaidi bali hata zina msimamo wa kindumakuwili kuhusiana nao.