Iran: Jamii ya kimataifa iwawajibishe ‘vinara wa mauaji ya kimbari’ wa Israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito wa kuwajibishwa "viongozi watenda jinai" wa utawala wa Israel kwa jinai zao dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, huku vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lililozingirwa vikiendelea bila kusitishwa.
Nasser Kan'ani alitoa wito huo jana Jumapili katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, akiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuizuia Israel kufanya uhalifu zaidi dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Kan'ani amemfananisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Adolf Hitler, dikteta wa zamanii wa Ujerumani, huku akilaani utepetevu wa jamii ya kimataifa ambao umepelekea kuendelezwa vita vya kikatili vya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.
“Karibu miongo minane baada ya kesi za Nuremberg, historia kwa mara nyingine tena inashuhudia kutokea kwa Hitler mwingine; Mhalifu anayeendeleza mauaji ya kimbari na mauaji ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Kipalestina katika kivuli cha kimya cha jamii ya kimataifa,” amesisitiza Nasser Kan’ani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: "Kama wale wanaodai kutetea haki za binadamu wanathamini ubinadamu na maisha ya binadamu, sasa ni wakati wa kuchukua hatua; kesho ni kuchelewa mno."
Amesisitiza kuwa, Jamii ya binadamu ina kiu ya ubinadamu na uadilifu zaidi kuliko wakati mwingine wowote na inataka kuhukumiwa vinara wa uhalifu wa utawala wa Kizayuni.
Karibu Wapalestina elfu 50 wameuawa na wengine zaidi ya laki moja wamejeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanya na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.