Makamu wa Rais wa Iran ahimiza kustawishwa uhusiano na Russia
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Iran amesema kuwa, viongozi wa ngazi za juu wa Iran wana nia ya kweli ya kustawisha uhusiano na Russia katika viwango vya juu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Mohammed Reza Aref, alisema hayo jana Jumatatu, wakati alipokutana na "Vitaly Saveliev" na "Alexey Overchuk" manaibu wawili wa Waziri Mkuu wa Russia hapa Tehran na kuongeza kuwa, suala la kustawishwa uhusiano wa Tehran na Moscow pamoja na kulindwa maslahi ya nchi hizo mbili lina manufaa kwa nchi zote za ukanda huu na kila mmoja ana wajibu wa kutumia uwezo uliopo kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa kadiri iwezekanavyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran aidha amesema kuwa, mbali na uhusiano wa pande mbili, Iran na Russia zinashirikiana pia katika jumuiya na taasisi muhimu za kimataifa kama vile Eurasia, BRICS na Shanghai na kwamba mazingira yote yanaruhusu kustawishwa zaidi ushirikiano wa nchi hizi mbili.
Kwa upande wao, manaibu wa Waziri Mkuu wa Russia wametilia mkazo azma ya nchi yao ya kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wamewasilisha ripoti kuhusu mchakato wa ufanikishaji wa miradi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na katika sekta ya mawasiliano na usafiri.
Viongozi hao wa ngazi za juu wa Russia wamegusia nafasi na uwezo muhimu wa kijiografia wa Iran na kusisitiza kuwa, Moscow ina nia ya kweli ya kuimarisha ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga zote.