Araqchi aipongeza Hamas kwa ushindi dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121558-araqchi_aipongeza_hamas_kwa_ushindi_dhidi_ya_israel
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameipongeza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa ushindi wa muqawama na wananchi wa Palestina dhidi ya Israel katika vita na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-01-17T14:03:19+00:00 )
Jan 17, 2025 14:03 UTC
  • Araqchi aipongeza Hamas kwa ushindi dhidi ya Israel

Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameipongeza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa ushindi wa muqawama na wananchi wa Palestina dhidi ya Israel katika vita na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.

Araqchi ameeleza haya katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Khalil al Hayya Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas baada ya kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita yaliyosubiriwa kwa muda mrefu ili kuhitimisha vita na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza.

Araqhchi amepongeza istiqama na kusimama imara wananchi wa  Palestina mkabala wa mauaji ya kimbari ya Israel na jinai zisizo na kifani za utawala huo ghasibu katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, mapambano ya Palestina yameulazimisha utawala ghasibu wa Israel kusalimu amri na kukubali kufikia makubaliano ya kusitisha vita na kubadilishana mateka.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Khalil al Hayya ameshukuru misaada na uungaji mkono wa uongozi, serikali  na wananchi wa Iran kwa Palestina na kupongeza uungaji mkono wa makundi ya Muqawama ya Lebanon, Yemen na Iraq kwa watu wa Palestina. 

Usitishaji huo wa mapigano, uliosimamiwa na Qatar ulitangazwa juzi Jumatano na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani.