Zarif asisitizia azma ya dhati ya Iran na Mali ya kushirikiana kiuchumi
Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mali zimeazimia kwa dhati kustawisha ushirikiano wa kiuchumi baina yao.
Dakta Zarif ameeleza hayo leo mjini Bamako katika kikao cha pamoja cha wadau wa sekta ya uchumi wa Iran na Mali na kuongeza kuwa: leo nchi hizi mbili zina azma ya dhati ya kustawisha uhusiano wao katika nyanja na sekta zote hususan ya uchumi na biashara.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa Mali ni nchi yenye umuhimu kwa Iran na kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu haitosita kutoa msaada wowote kwa wananchi wa nchi hiyo.
Dakta Zarif ameashiria kuwepo wadau wa sekta za binafsi na serikali za Iran walioandamana naye katika safari yake nchini Mali na kubainisha kuwa: ujumbe wa kiuchumi alioandamana nao katika safari yake barani Afrika ni ujumbe mkubwa unaojumuisha wadau wa sekta tofauti ikiwemo ya ujenzi wa barabara na mabwawa, nishati, sayansi na teknolojia, afya na masuala ya benki.
Mali ni kituo cha mwisho cha safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika ya Magharibi.
Kabla ya kuelekea Mali, Dakta Zarif alikuwa tayari amezitembelea Ghana, Nigeria na Guinea Conakry na kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo.../