Iran: Kuzishutumu nchi huru bila ya sababu ni kuendeleza uvunjaji wa sheria
(last modified Fri, 24 Jan 2025 03:37:00 GMT )
Jan 24, 2025 03:37 UTC
  • Iran: Kuzishutumu nchi huru bila ya sababu ni kuendeleza uvunjaji wa sheria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, tuhuma ya Marekani dhidi ya Cuba na kuliingiza tena jina la nchi hiyo katika orodha ya mataifa yanayodaiwa kuunga mkono ugaidi ni hatua ya kipuuzi na isiyokubalika kabisa.

Ismail Baghaei Hamaneh alisema hayo jana Alkhamisi wakati akionesha hisia zake kufuatia kitendo cha kibeberu cha Washington cha kuliingiza tena jina la Cuba kwenye orodha ya nchi ambazo Marekani inadai zinaunga mkono ugaidi na kuongeza kwamba, hatua ya nchi moja kujipa haki ya kuainisha nini ugaidi na nani anaunga mkono ugaidi ni kitendo cha kipuuzi na kibeberu bali pia ni kuzivunjia heshima nchi huru duniani. 

Baqaei Hamaneh amesema kuwa, hatua hiyo ya Marekani ni kinyume na misingi na sheria za kimataifa na ni kisingizio cha kuweka vikwazo vya upande mmoja na vya kikatili dhidi ya mataifa huru. Amesisitiza kuwa, hatua hizo za kibeberu za Marekani si tu zinakanyaga haki za kimsingi za binadamu lakini pia zinapuuza maamuzi ya wananchi wa Cuba na uhuru wao wa kujiamulia wenyewe mambo yao. 

Rais mpya wa Marekani, Donald Trump amebatilisha uamuzi wa Rais wa zamani Joe Biden wa kuiondoa Cuba katika orodha ya mataifa yanayodaiwa na Marekani kuwa eti yanafadhili ugaidi.

Wiki iliyopita na katika hatua iliyochelewa, utawala wa Biden uliiondoa Cuba kwenye orodha ya Marekani ya nchi zinazodaiwa kufadhili ugaidi. 

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amejibu hatua hiyo akisema kwamba, rais mpya wa Marekani ni mtu mwenye majigambo na kiburi kupindukia hivyo hatua yake hiyo haishangazi na wala haiitetereshi Duba.