Ayatullah Khatami: Iran itatoa jibu kali kwa ukwamishaji wa Marekani kuhusu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21091-ayatullah_khatami_iran_itatoa_jibu_kali_kwa_ukwamishaji_wa_marekani_kuhusu_jcpoa
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran ameeleza kuwa jibu litakalotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa njama na ukwamishaji unaofanywa na Marekani kuhusu Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA litakuwa kali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2016 10:40 UTC
  • Ayatullah Khatami: Iran itatoa jibu kali kwa ukwamishaji wa Marekani kuhusu JCPOA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran ameeleza kuwa jibu litakalotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa njama na ukwamishaji unaofanywa na Marekani kuhusu Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA litakuwa kali.

Akihutubia katika Sala ya Ijumaa hapa Tehran, Ayatullah Ahmad Khatami amesema kuwa hatua ya Congresi ya Marekani ya kurefusha na kupasisha vikwazo kwa muda wa miaka kumi dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa muafaka wa JCPOA ambao unatambuliwa kuwa ni makubaliano ya kimataifa na kuongeza kuwa, kutotekeleza ahadi Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 kumethibitisha kuwa, nchi hiyo haiheshimu wala kufungamana na ahadi zake katika uga wa kimataifa. 

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran amemnasihi Barak Obama Rais wa Marekani anayemaliza muda wake kwamba, ataacha jina jeusi katika historia yake iwapo ataathiriwa na lobi ya Wazayuni  na kuafiki kura za Congresi ya nchi hiyo ili kurefusha vikwazo dhidi ya Iran. 

Ayatullah Ahmad Khatami akisalisha Sala ya Ijumaa Tehran 

Ayatullah Khatami amejibu matamshi dhidi ya Iran yaliyotolewa na Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza  katika kikao cha juzi cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Manama mji mkuu wa Bahrain kuhusu hatua ya London ya kutangaza kushirikiana na nchi za Kiarabu dhidi ya Iran kwamba, hadi leo hii Uingereza haijaacha kufanya jitihada za kupambana na Uislamu na kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya nchi za Kiislamu. Khatibu wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran amesema, matamshi hayo yasiyo na msingi ya Waziri Mkuu wa Uingereza yanatokana na matatizo iliyonayo nchi hiyo katika uhusiano wake na Umoja wa Ulaya na kwamba, kuendelea miamala kama hiyo kutaifanya hali ya London kuwa tata zaidi.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi Theresa May akiwa na viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Manama 

Ayatullah Ahmad Khatami amebainisha kuwa, wananchi wamoja wa Iran chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu watazuia njama zinazofanywa na madola ajinabi dhidi ya taifa hilo kwa kuwa kwao imara. Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Tehran ameashiria pia ushindi wa hivi karibuni wa majeshi ya Syria na Iraq na wananchi wa nchi mbili hizo dhidi ya magaidi na kueleza matarajio yake kuwa, makundi ya kigaidi hivi karibuni yataangamizwa kabisa katika nchi hizo. Ayatullah Khatami ameashiria vile vile kuhusu kukaribia Iran katika kipindi cha uchaguzi na kueleza kuwa, uchaguzi ni uhai wa kiaisasa na dhihirisho la kuwepo uhuru hapa nchini; ambao wamezawadiwa watu wa nchi kwa baraka za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.