Spika Larijani: Marekani imesibiwa na hali ya kujihofu yenyewe
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya karibuni ya serikali mpya ya Marekani ya kufuta utoaji viza kwa raia wa Iran inadhihirisha udhaifu na uduni wa mitazamo na mwenendo wa viongozi wa serikali hiyo.
Ali Larijani ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa kikao cha kawaida cha bunge na kuongeza kuwa hatua ya serikali ya Marekani ya kufuta utoaji viza kwa raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu na hasa raia wa Iran imeonesha hulka ya kikatili na ya kibaguzi ya viongozi wake iliyojificha nyuma ya pazia la kuhadaa watu, la kutetea demokrasia na haki za binadamu.
Spika wa Bunge amesema, kulitaja jina la Iran kwa kisingizio cha hofu ya kuchelea vitendo vya kigaidi inafanana zaidi na utani na kichekesho na kubainisha kuwa hakuna asiyejua kuwa katika miaka yote hii Iran imesimama kwa nguvu zake zote kupambana na magaidi.
Dakta Larijani ameongeza kuwa serikali ya Marekani, sasa imesibiwa na hali ya sutafahamu na ya kujihofu yenyewe. Aidha amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma thabiti ya kupambana na ugaidi na wala haitoathiriwa na usanii wa kitoto wa baadhi ya nchi…/