Iran yamwita balozi wa Uswisi kulalamikia Marekani kuwapiga marufuku Waislamu
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita Balozi wa Usiwis mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko rasmi kufuatia hatua ya rais wa Marekani kupitisha sheria za kibaguzi za kuwazuia raia wa Iran na nchi zingine sita za Kiislamu kuingia nchini humo.
Katika mkutano huo wa Jumapili, Mkurugenzi wa Masuala ya Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Mohammad Keshavarz-Zadeh, amemkabidhi Balozi wa Uswisi mjini Tehran, Giulio Haas, barua rasmi ya malalamiko dhidi ya Marekani. Ubalozi wa Uswisi mjini Tehran ndio unaowakilisha maslahi ya Marekani nchini Iran.
Mwanadiplomasia huyo wa Uswisi amefahamishwa kuwa hatua ya rais Donald Trump wa Marekani kuwapiga marufuku Waislamu kuingia nchini humo ni ya kibaguzi, haikubaliki na inakiuka mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu pamoja na mapatano yaliyotiwa saini kuhusu masuala ya visa baina ya Tehran na Washington Agosti mwaka 1955.
Keshavarz-Zadeh amemfahamisha balozi wa Uswisi kuwa, kuna umuhimu wa kulindwa haki za raia Wairani na kuongeza kuwa, Wairani wamekuwa waathirika wa makundi ya kigaidi yanayopata himaya ya Marekani kwa miongo kadhaa sasa. Aidha amesema Wairani hawajawahi kuhusika na oparesheni yoyote ya makundi ya kigaidi.
Balozi wa Uswisi mjini Tehran amesema ana habari kuhusu amri hiyo ya Trump kuhusu Iran na kuongeza kuwa atawasilisha malalamiko ya Iran kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.