Qassemi alaani shambulio la kigaidi katika kituo cha Kiislamu Canada
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulizi la kigaidi lililofanywa dhidi ya kituo cha Kiislamu huko Quebec nchini Canada.
Bahram Qassemi amelitaja shambulio la kigaidi lililofanywa katika msikiti mkuu na Kituo cha Utamaduni cha Kiislamu huko Quebec nchini Canada kuwa ni jinai na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria tishio na hatari ya ugaidi duniani na vitendo vya uchupaji mipaka kuwa visivyotambui mipaka yoyote na kueleza kuwa, ugaidi haufungamani na eneo moja au nchi kadhaa bali nchi zote duniani zinaweza kulengwa na hujuma na jinai za makundi ya kigaidi.
Qassemi amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuwepo azma ya kweli ya kimataifa ili kuzuia kuenea na kuimarika fikra za kuchupa mipaka na misimamo mikali, na vilevile kushirikiana nchi zote katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.
Watu sita waliuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa Jumapili usiku katika msikiti wa Quebec, Canada wakati Waislamu walipokuwa wakitekeleza ibada ya Swala.