Rouhani: Ushirikiano wa kimataifa unahitajika kukabili ugaidi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ushirikiano wa kimataifa unahitajika iwapo dunia inataka natija katika vita dhidi ya ugaidi.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumanne katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Iran kama muhanga wa harakati za kigaidi, imekuwa katika mstari wa mbele kukabiliana na jinamizi hilo kwa hali na mali na kusisitiza kuwa sharti nchi za dunia zishirikiane ili kuushinda ugaidi.
Akiashiria juhudi za serikali na taifa la Syria katika vita dhidi ya ugaidi, Dakta Hassan Rouhani amekariri kuwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu hauhitaji suluhu ya kijeshi bali ya kisiasa huku akiitaka Ufaransa na jamii ya kimataifa kwa ujumla kutuma misaada ya kibinadamu kwa watu wa Syria.
Kwengineko katika mazungumzo na Jean-Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitizia haja ya kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.
Rais Rouhani amebainisha kuwa, kufikiwa makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Marekani, China, Russia, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani kulikuwa nukta muhimu katika siasa za kimataifa, na kwamba kutekelezwa kwake ni muhimu zaidi kuliko maandishi ya makubaliano hayo.
Kwa upande wake, Jean-Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuna udharura wa pande zote kutekeleza makubaliano hayo kwa nia njema. Mbali na kupongeza nafasi ya Iran kieneo na kimataifa, afisa huyo wa ngazi za juu wa Ufaransa amesema Umoja wa Ulaya EU unafanya juu chini kuja na stratejia moja ya kuhakikisha kuwa makubaliano hayo ya nyuklia ya Vienna yanaheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu.