Iran ya Kiislamu imevunja njama zote za maadui wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25268-iran_ya_kiislamu_imevunja_njama_zote_za_maadui_wake
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema kuwa uwezo wa Iran ya Kiislamu ndio uliovunja njama zote za maadui dhidi ya nchi hii.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Feb 17, 2017 11:01 UTC
  • Iran ya Kiislamu imevunja njama zote za maadui wake

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema kuwa uwezo wa Iran ya Kiislamu ndio uliovunja njama zote za maadui dhidi ya nchi hii.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim  Siddiquie Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria madai ya kiongozi mmoja wa Ulaya aliyesema kuwa iwapo Iran haingetia saini mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama JCPOA basi nchi hii ingeshambuliwa kijeshi na kusema madai hayo ni uongo mtupu.  Sheikh Sidduquie amesema dunia haina uwezo wa kupigana na Iran na kwamba taifa la Iran litasimama kidete dhidi ya adui hadi mwisho.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ameongeza kuwa, iwapo Marekani na madola mengine makubwa ya kibeberu hayajaweza kushambulia Iran kijeshi, hilo limetokana na uwezo wa taifa na nguvu za kijeshi za Iran. Hujjatul Islam wal Muslimin Siddiquie amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya saba kwa uwezo wa kijeshi duniani.

Sala ya Ijumaa Tehran

Aidha amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwa macho kuhusu vita vya kiuchumi na kiutamaduni dhidi ya Iran ya Kiislamu na kusema, kutekelezwa kikamilifu sera ya uchumi wa kimapambano ni jambo ambalo litasambaratisha njama hizo za adui.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran pia amelaani vikali utawala wa kiimla wa Aal Khalifa nchini Bahrain kwa kuendelea kukandamiza wananchi wanamapinduzi nchini humo na kuongeza kuwa, hakuna ukandamizaji utakaozima mwamako wa wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala kibaraka wa Aal Khalifa na kwamba hatimaye wananchi watapata ushindi. Hali kadhalila Sheikh Siddiquie ameulaani vikali Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kunyamazia kimya jinai za utawala wa Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen.