Abdollahian: Kukombolewa mji wa Palmyra ni ishara kuwa magaidi wamefikia mwisho wao
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu nchini Iran (Bunge) katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, kukombolewa kikamilifu mji wa kihistoria wa Palmyra katika mkoa wa Homs, magharibi mwa Syria, ni ishara ya wazi kwamba magaidi wamefikia mstari wa mwisho wa uhai wao.
Hossein Amir-Abdollahian sambamba na kutoa pongezi kwa jeshi la serikali na taifa la Syria juu ya kukombolewa mji huo muhimu wa kihistoria amesema kuwa, utatuzi wa masuala ya nchi hiyo kamwe hauwezi kufikiwa kwa mtutu wa bunduki, ispokuwa tu kama magaidi watakubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya mjini Geneva, Uswisi.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo daima imekuwa muungaji mkono mkubwa wa serikali ya Syria, itaendelea kufanya hivyo kwa kuwa nchi hiyo (Syria) ipo katika mstari wa uungaji mkono kwa harakati za kukombolewa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa utawala ghasibu wa Kizayuni. Alkhamis ya jana jeshi la Syria lilitangaza habari ya kukombolewa kikamilifu mji wa kihistoria wa Palmyra kutoka mikononi mwa wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS.)
Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya kuibuka mgogoro wa Syria hapo mwaka 2011, magaidi wakufurishaji wanaopata himaya kutoka Saudia, Israel, Marekani na waitifaki wao ikiwemo Uturuki kwa ajili ya kutaka kuiondoa madarakani serikali ya kisheria ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo, walianza kudhibiti miji muhimu ikiwemo ya Homs, Aleppo na maeneo mengine ya taifa hilo la Kiarabu.