Zarif: Israel ndio tishio kubwa zaidi la nyuklia duniani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel ni "tishio kubwa zaidi la nyuklia" dhidi ya eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen ya Lebanon.
Ameashiria tishio la nyuklia la Israel dhidi ya eneo na dunia na kueleza kwamba siasa za Israel kuhusu mataifa ya eneo zimekuwa ni za kiadui; na lengo la uchukuaji misimamo ya vitisho unaofanywa na utawala huo ni "kuficha ukweli" kwa ajili ya kufanikisha sera zake za kivamizi.
Waziri Zarif amezungumzia pia husiano wa Iran na Saudi Arabia na kueleza kwamba Tehran inaweza kuwa na uhusiano mzuri na Riyadh. Amefafanua kwa kusema: "Iran iko tayari kushirikiana na nchi zote za Kiislamu kwa msingi wa kufuata sera za kutoanzisha uchokozi na kuingilia masuala ya ndani. Ushirikiano wetu na majirani zetu ikiwemo Saudia unapasa uwe na lengo la kuleta amani Bahrain, Yemen na Syria".
Aidha ameiasa Saudia kwa kusema: "Naishauri Saudi Arabia, badala ya kujiweka karibu na wengine kwa ajili ya kuidhuru Iran ishirikiane nasi. Nchi zinazofanya makosa zijilaumu zenyewe na si kuilaumu Iran. Si kosa letu sisi kwamba nchi nyengine zinaamua bila ya sababu kuivamia Yemen na kuunga mkono Daesh na Jabhatu-Nusra nchini Syria".
Katika mahojiano hayo Waziri Zarif aidha ameeleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya nchi za Kiislamu kuwa katika safu moja na nchi nyengine ili kuzifanyia uadui nchi nyengine za Kiislamu…/