Russia: Iran ni mshirika wa aina yake katika vita dhidi ya ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27102-russia_iran_ni_mshirika_wa_aina_yake_katika_vita_dhidi_ya_ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amepuuzilia mbali madai bandia kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni mshirika mkubwa katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2017 10:30 UTC
  • Russia: Iran ni mshirika wa aina yake katika vita dhidi ya ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amepuuzilia mbali madai bandia kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni mshirika mkubwa katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi nchini Syria.

Katika mahojiano na jarida la Marekani la National Interest, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema madai hayo yanayotolewa na Washington na waitifaki wake hayana msingi na hakuna ushahidi wowote unaoweza kuzipa mashiko tuhuma hizo.

Lavrov amebainisha kuwa: "Tunachokijua kuihusu Iran ni kwamba taifa hilo ni mdau mkubwa katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi nchini Syria kwa mwaliko wa serikali ya Damascus."

Iran, Russia na Hizbullah zinashirikiana kuzima ugaidi Syria

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia ameongeza kuwa, mbali na kuliunga mkono jeshi la Syria katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi nchini humo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashirikiana kwa karibu na harakati ya Hizbullah ya Lebanon, ambayo pia inashiriki 'kihalali' katika operesheni za kuyatokomeza magenge ya kigaidi Syria.

Matamshi ya Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ni jibu kwa tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na maafisa wengine wa serikali ya Washington wakidai kwamba Iran ni mfadhili mkuu wa ugaidi duniani.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa ushauri wa kijeshi kwa vikosi vya jeshi la Syria kwa ombi la serikali ya Damascus, katika operesheni zake dhidi ya magenge ya kigaidi.