Larijani: Lengo la makundi ya kigaidi ni kuzusha udini duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27628-larijani_lengo_la_makundi_ya_kigaidi_ni_kuzusha_udini_duniani
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi dhidi ya makanisa mawili nchini Misri siku ya Jumapili iliyopita ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa huku akisisitiza kuwa, lengo la magaidi ni kuzusha mifarakano ya kidini duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 11, 2017 15:22 UTC
  • Larijani: Lengo la makundi ya kigaidi ni kuzusha udini duniani

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi dhidi ya makanisa mawili nchini Misri siku ya Jumapili iliyopita ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa huku akisisitiza kuwa, lengo la magaidi ni kuzusha mifarakano ya kidini duniani.

Katika barua yake ya salamu za rambirambi kwa  Ali Abdel Aal, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Misri, Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran amesema ugaidi, jinamizi ambalo ni tishio kwa watu wa dini zote, unakinzana na thamani zote za utu na mafundisho ya kiroho.

Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga, serikali na taifa la Misri kwa ujumla kufuatia hujuma hizo za kikatili, Larijani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kusimama na Wamisri katika juhudi za kuutokomeza ugaidi.

Kanisa la Kikhufti lililoshambuliwa na Daesh Jumapili

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, harakati za kigaidi duniani zinaweza kuzimwa tu kwa ushirikiano na mashauriano ya serikali za eneo la Mashariki ya Kati na kimataifa.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh waliwalenga kwa mabomu Wakristo ambao walikuwa wanaadhimisha Jumapili ya Matawi, katika Kanisa la Kikhufti (Coptic) mjini Tanta na kanisa jingine katika mji wa Alexandria, eneo la Nile Delta ambapo watu 49 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa. 

Hii ni katika hali ambayo, Waislamu nchini Misri tangu jana wamekuwa wakikusanyika katika misikiti na vituo mbalimbali kutoa damu, kwa ajili ya majeruhi wa ukatili wa Daesh.