Ayatullah Khatami: Bahrain imegeuzwa kuwa jela kubwa ya wananchi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29624-ayatullah_khatami_bahrain_imegeuzwa_kuwa_jela_kubwa_ya_wananchi
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran sambamba na kulaani hujuma na uvamizi wa vikosi vya usalama vya Bahrain dhidi ya nyumba ya Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo ametangaza kuwa, utawala wa Aal khalifa kwa kufanya ukandamizaji, kamatakamata na aina mbalimbali za jinai, umeigeuza nchi hiyo na kuwa jela kubwa kwa ajili ya wananchi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 26, 2017 09:31 UTC

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran sambamba na kulaani hujuma na uvamizi wa vikosi vya usalama vya Bahrain dhidi ya nyumba ya Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo ametangaza kuwa, utawala wa Aal khalifa kwa kufanya ukandamizaji, kamatakamata na aina mbalimbali za jinai, umeigeuza nchi hiyo na kuwa jela kubwa kwa ajili ya wananchi.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika hotuba za Swala ya Ijumaa mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala hiyo ya kimaanawi na kisiasa mjini Tehran na kubainisha kwamba, unyama wa utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wananchi ambao haujawahi kushuhudiwa unafanyika kwa himaya ya Marekani na Saudi Arabia.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, uvamizi na shambulio la vikosi vya usalama vya Bahrain dhidi ya makazi ya Sheikh Issa Qassim ni kisingizio cha kukabiliana na Uislamu asili ulioletwa na Mtume Muhammad saw.

Wananchi wa Iran wakifanya maandamano ya kumtetea Sheikh Issa Qassim wa Bahrain

Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, watawala wa Bahrain ni dhihirisho la Uislamu wa Marekani.

Ayatullah Khatami amelaani pia hujuma na mashambulio  ya vikosi vya usalama vya Saudi Arabia dhidi ya mji wa al-Awamiyah ambao wakazi wake ni Waislamu wa Kishia mashariki mwa nchi hiyo.

Kadhalika khatibu wa Swala ya Ijumaa ya wiki hii hapa mjini Tehran ameashiria mkutano wa hivi karibuni wa viongozi wa Kiarabu na Rais Donald Trump wa Marekani huko Riyadh Saudi Arabia na kusema kuwa, watawala vibaraka na tegemezi watakumbwa na hatima kama iliyompata dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.