Kiongozi Muadhamu: Nchi zinazojitegmea zishirikiane zaidi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito wa kushirikiana zaidi nchi zinazojitegemea duniani.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameyasema hayo leo alasiri mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Truong Tan Sang wa Vietnam. Katika kikao hicho Kiongozi Muadhamu amesema miongoni mwa sera muhimu za Iran ni kushirikiana na nchi za Asia, Vietnam ikiwemo. Ameongeza kuwa Vietnam imekuwa ikishirikiana na Iran katika uga wa kimataifa na kwa msingi huo ushirikiano wa nchi mbili unapaswa kuimarishwa zaidi. Kiongozi Muadhamu amesema: "Ushujaa na mapambano ya taifa la Vietnam na shakhsia wake wakubwa kama vile Ho Chi Minh na Jenerali Giap ambapo walikabiliana na kupambana na wavamizi wa kigeni ni jambo ambalo limelifanya taifa la Vietnam liheshimike na liwe na hadhi mbele ya taifa la Iran. "Mfungamano huu unapaswa kuandaa mazingira mwafaka ya kuimarisha zaidi uhusiano", amesisitiza Ayatullah Khamenei.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama za madola makubwa duniani kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine na kusema: "Uingiliaji huu mara nyingine hufanyika kwa njia ya kuanzisha vita kama vita vya Vietnam na wakati mwingine hufanyika kwa kutumia mbinu nyinginezo; njia ya kukabiliana na uingiliaji huo ni kushirikiana na kukurubiana zaidi nchi zenye misimamo huru."
Kwa upande wake, Rais Truong Tan Sang wa Vietnam ameishukuru Iran kwa kuiunga mkono Vietnam katika nyuga za kimataifa. Amesema Vietnam nayo pia inaunga mkono misimamo ya Iran katika uga wa kimataifa na kwamba nchi yake inaamini kwamba kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ni haki isiyopingika ya Iran na katika siku za usoni Vietnam itaendelea kuiunga mkono Iran.
Aidha amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuenzi mapambano na viongozi wa Vietnam waliopambana na wavamizi wa kigeni. Amesema watu wa Vietnam kwa miaka kadhaa walipambana na wavamizi wa kigeni hadi kupata uhuru na kujitegemea.
Aidha amesisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Vietnam. Amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fremu ya sera zake za kutizama Mashariki, sawa na huko nyuma inaitazama Vietnam kama mshirika muhimu."