Iran: Tupo tayari kutuma dawa na timu ya madaktari Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32186-iran_tupo_tayari_kutuma_dawa_na_timu_ya_madaktari_palestina
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) katika Masuala ya Kimataifa amesema Iran iko tayari kutuma dawa ili kuwasaidia haraka raia wa Kipalestina waliojeruhiwa hivi karibuni na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika msikiti wa al Aqsa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2017 02:39 UTC
  • Iran: Tupo tayari kutuma dawa na timu ya madaktari Palestina

Msaidizi Maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) katika Masuala ya Kimataifa amesema Iran iko tayari kutuma dawa ili kuwasaidia haraka raia wa Kipalestina waliojeruhiwa hivi karibuni na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika msikiti wa al Aqsa.

Hussein Amir Abdulahiyan ameeleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Quds na katika maeneo ya kandokando na msikiti wa al Aqsa na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutuma haraka misaada ya madawa na ya kiafya sambamba na kutuma timu ya madaktari kwa ajili ya kuwatibu majeruhi wa Kipalestina. Abdulahiyan aliyasema hayo jana hapa Tehran katika mazungumzo na Khalid al Qaddumi Mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina Hamas hapa Tehran.  

Amir Abdulahiyan ameashiria uhusiano uliopo kati ya Sekretariati ya Mkutano wa Kimataifa wa Kuiunga Mkono Intifadha ya Paletina na karibu taasisi 800 za kimataifa za kiraia na kubainisha wazi hatua zinazotekelezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuwaunga mkono raia wa Palestina na kuwepo udharura wa kuulinda msikiti mtukufu wa al Aqsa.

Katika mazungumzo hayo naye Mwakilishi wa Harakati ya Hamas hapa Tehran ameitaja hatua ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni ya kuwakandamiza Wapalestina kuwa ni kisingizio kwa ajili ya kuukalia tena msikiti wa al Aqsa na kuongeza kuwa, Wapalestina watatoa jibu kali kwa Tel Aviv kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni.  

Wapalestina wakikimbia risasi za wanajeshi wa Israel nje ya lango la Lion katika msikiti mtakatifu wa al Aqsa 

Ijumaa iliyopita ya tarehe 21 Julai raia wa Palestina walipambana na wanajeshi wa Kizayuni wakipinga mashambulizi ya utawala huo ghasibu katika msikiti wa al Aqsa na kuweka milango eti ya usalama katika maeneo ya kuingilia msikitini hapo; mapigano yaliyosababisha kuuliwa shahidi Wapalestina wasiopungua wanne na kujeruhiwa wengine karibu 400.