Iran yaitaka Marekani iache kuingilia masuala ya magharibi mwa Asia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33586-iran_yaitaka_marekani_iache_kuingilia_masuala_ya_magharibi_mwa_asia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali mikakati mipya ya Marekani nchini Pakistan na kuitaka Washington iache mara moja kuingilia masuala ya nchi nyingine.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Aug 24, 2017 23:54 UTC
  • Iran yaitaka Marekani iache kuingilia masuala ya magharibi mwa Asia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali mikakati mipya ya Marekani nchini Pakistan na kuitaka Washington iache mara moja kuingilia masuala ya nchi nyingine.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Bahram Qassemi akisema hayo jana usiku na kuongeza kuwa, matatizo yaliyopo leo katika eneo la magharibi mwa Asia yanatokana na siasa ghalati na mbovu za Marekani kwenye eneo hilo hususan nchini Afghanistan na kwamba matunda ya uingilia wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi za eneo hili si kitu kingine isipokuwa kuongezeka machafuko, vurugu, wasiwasi, vitendo vya kigaidi na misimamo ya kuchupa mipaka.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema, Marekani haina haki ya kuzipangia nchi nyingine nini cha kufanya na kwamba nchi za eneo hili zina uwezo wa kutosha wa kutatua masuala yao kupitia ushirikiano baina yao bila ya uingiliaji wa madola ya kigeni kama ambavyo hazina haja kabisa na mikakati mipya ya Marekani ambayo lengo lake ni kuvuruga utulivu na kulea magaidi.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 21 Agosti, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza mikakati mipya ya Washington ya eti kupambana na ugaidi na kudai kuwa Pakistan ni maficho salama ya magaidi wanaohatarisha usalama wa Afghanistan.

Tuhuma hizo zimetolewa wakati ni Marekani ndiyo iliyoivamia Afghanistan mwaka 2001 kwa madai ya kupambana na magaidi walioshiriki katika mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani. Licha ya kupita miaka 16 tangu wakati huo, lakini si tu Marekani imeshindwa kuwamaliza magaidi, bali ukosefu wa amani umeongezeka sana ndani na nje ya Aghanistan.