Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aelekea Uturuki
Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameelekea Uturuki hii leo ambapo atafanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Ankara.
Zarif anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan, Waziri Mkuu Ahmed Davutoglu baada ya kufanya kikao na mwenzake Mevlut Cavusoglu. Mazungumzo kati ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na viongozi wa Uturuki yanatazamiwa kujikita katika masuala ya kuimarisha ushikirkiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa.
Safari ya Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajiri siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmed Davutoglu kuitembelea Iran na kufanya mazungumzo na viongozi nchini, akiwemo Rais Hassan Rouhani. Katika kikao hicho cha Machi 6, Rais Hassan Rouhani alisema kuwa, Iran na Uturuki zinapaswa kuwa na ushirikiano, uratibu zaidi na kuelekeza nguvu zao katika vita dhidi ya ugaidi ukiwa kama ni adui wa pamoja na hivyo kuimarisha misingi ya amani na uthabiti. Kwa upande wake Ahmed Davutoglu, Waziri Mkuu wa Uturuki alisisitiza kwamba, nchi yake imeazimia kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.