Iran yatoa jibu kwa matamshi ya kilaghai ya Netanyahu katika UNGA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34593-iran_yatoa_jibu_kwa_matamshi_ya_kilaghai_ya_netanyahu_katika_unga
Mshauri wa ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema matamshi dhidi ya Iran aliyotoa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni ya kinafiki na ya kilaghai.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 20, 2017 02:58 UTC
  • Iran yatoa jibu kwa matamshi ya kilaghai ya Netanyahu katika UNGA

Mshauri wa ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema matamshi dhidi ya Iran aliyotoa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni ya kinafiki na ya kilaghai.

Katika hotuba yake aliyotoa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Banjamin Netanyahu amerudia madai yake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutaka makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yabatilishwe au yafanyiwe mabadiliko.

Kuhusiana na matamshi hayo ya Netenyahu, Hossein Maleki, mshauri wa ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, upinzani wa utawala wa Kizayuni kwa makubaliano ya JCPOA unatokana na dhati halisi ya utawala huo ya kupinga diplomasia na badala yake kuunga mkono vita na mapigano tu ambavyo ndiyo msingi wa kuasisiwa utawala huo haramu. 

Benjamin Netanyahu

Maleki amebainisha kuwa Netanyahu anapaswa kutoa jibu kwa hatua za utawala wa Kizayuni za kuanzisha zaidi ya vita 15, kukiuka makumi ya maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na maazimio yapatayo 100 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuunga mkono ugaidi kwa silaha na zana za kivita, kufanya mauaji ya kimbari, jinai dhidi ya binadamu, ubomoaji nyumba, skuli na hospitali, mauaji ya Sabra na Shatila pamoja na mauaji, utiaji nguvuni na kuwaweka gerezani maelfu ya Wapalestina.

Mshauri wa ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba licha ya utawala wa Kizayuni kuwa na silaha za kisasa zaidi za mauaji ya halaiki zikiwemo za kemikali, vijidudu na nyuklia hauko tayari kujiunga na Mkataba Unaopiga Marufuku Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT) na unapinga Mashariki ya Kati kufanywa eneo lisilo na silaha za nyuklia.../