Iran yafanyia majaribio kombora jipya la balistiki
Iran imefanyia majaribio yaliyofana kombora lake jipya la masafa marefu la balistiki linalojulikana kama Khorramshahr, masaa machache tu baada ya kulizindua katika gwaride la kijeshi mjini Tehran.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limeonyesha taswira za kombora hilo likifanyiwa majaribio Ijumaa katika sehemu isiyojulikana.
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amesema kuwa, kombora hilo la balestiki lina uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 2000 na uwezo wa kubeba vichwa kadhaa vya makombora.
Brigedia Jenerali Hajizadeh amesema, kombora hilo la Khorramshahr limefanywa dogo kwa umbo lakini lenye uwezo mkubwa wa kitaktiki na lwamba litaanza kutumika katika siku kadhaa zijazo.
Kombora la Khorramshahr, ni aina ya tatu ya makombora ya Iran yenye uwezo wa kulenga shabaha umbali wa kilomita 2000. Makombora mengine ni Qadr-F na Sejjil.
Akizungumza jana katika gwaride la Wiki ya Kujihami Kutakatifu mjini Tehran, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema kuwa, uwezo mkubwa wa jeshi la nchi hii haujawahi kutumiwa katika kuzivamia nchi nyingine, katika hali ambayo madola ya kibeberu yanamwaga silaha za maangamizi katika eneo hili la Mashariki ya Kati ili kuvuruga amani na utulivu.