Rais Rouhani: Marekani imezidi kujidhalilisha kwa kukataa kuheshimu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38971-rais_rouhani_marekani_imezidi_kujidhalilisha_kwa_kukataa_kuheshimu_jcpoa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani imefeli kimataifa na katika uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2018 12:27 UTC

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani imefeli kimataifa na katika uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Iran.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika sherehe za kufunga Tamasha la Tisa la Kimataifa la Farabi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Wamarekani wameshindwa vibaya mara mbili na taifa la Iran, kwanza kutokana na Marekani kukanyaga maafikiano ya kimataifa ya JCPOA na pili katika kuingilia kwake masuala ya ndani ya Iran kiasi kwamba fikra za walio wengi duniani leo zimesimama kukabiliana na Marekani.

Rais Hassan Rouhani akihutubia Tamasha la Tisa la Kimataifa la Farabi

 

Amesema, Wamarekani wameshindwa kuwaburuza walimwengu licha ya kutumia ubeberu, udikteta, kiburi na kujiona bora na kusisitiza kuwa, kufeli huko vibaya Marekani ni mafanikio makubwa kwa taifa la Iran. Aidha amesema, Iran imepata mafanikio katika maafikiano ya nyuklia ya JCPOA na hakuna mtu anayeweza kuyafuta mafanikio hayo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuwa, Tehran haijawahi hata mara moja kufuatilia kumiliki silaha za nyuklia na imeweza kulithibitisha hilo katika hatua zote za mafungumzo.  Amesema, nchi zote katika azimio la Umoja wa Mataifa zimekiri kuwa Iran ina haki ya kuendelea kufanya utafiti na kuimarisha miradi yake ya amani ya nyuklia, hivyo ushindi kama huu hauwezi kupotea wakati wowote ule.

Vile vile amegusia namna baadhi ya nchi zinavyozusha migogoro na machafuko na kufanya jinai za kila namna katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, wale walioitumbukiza Mashariki ya Kati katika machafuko hawana welewa sahihi kuhusiana na masuala ya kijamii ya eneo hili na wanatumia vibaya maendeleo ya kiteknolojia kuzusha machafuko na migogoro katika jamii za mataifa mengine.