Muungano wa Saudia, Imarati na Bahrain huko Davos, ni kosa la kistratajia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39537-muungano_wa_saudia_imarati_na_bahrain_huko_davos_ni_kosa_la_kistratajia
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameutaja muungano eti dhidi ya Iran wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain katika Mkutano wa Kimataifa wa uchumi huko Davos nchini Uswisi kama kosa la kistratajia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2018 04:15 UTC
  • Muungano wa Saudia, Imarati na Bahrain huko Davos, ni kosa la kistratajia

Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameutaja muungano eti dhidi ya Iran wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain katika Mkutano wa Kimataifa wa uchumi huko Davos nchini Uswisi kama kosa la kistratajia.

Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawaheshimu majirani na ndugu zake Waislamu katika eneo hili.

Ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "Katika hali ambayo Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zina mambo kadhaa ya kufanana na yanayoweza kuzileta pamoja, lakini baadhi yazo zimekubali kutumiwa kama karatasi shashi na Ikulu ya Marekani White House na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad."

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran ameyakumbusha mataifa hayo ya Kiarabu namna yalivyorubuniwa na Marekani katika miaka ya 80 na 90 na kusema kuwa, "Msisahau siku zilizojaa changamoto zama za Saddam (Hussein) wakati alipoivamia Kuwait, tulisimama kidete na jirani zetu hao wa Kiarabu na kuwaunga mkono ndugu zetu wa Kuwait."

Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa Davos

Itakumbukwa kuwa, maafisa wa nchi hizo za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi siku ya Jumatano walitumia jukwaa la mkutano wa Davos kuiponda Iran na kuitaka Tehran iache eti tabia yake ya kuvuruga uthabiti katika eneo.

Maafisa hao wa Kiarabu walitumia fursa hiyo kutokana na Iran kutotuma mwakilishi katika mkutano huo wa uchumi nchini Uswisi.